Favoriten auf Augenhöhe
6 Juni 2012Mara ya kwanza Ujerumani ilionja chungu ya kipigo dhidi ya Uhispania katika fainali ya kombe la mataifa ya Ulaya mwaka 2008 wakati Austria na Uswisi zilipokuwa wenyeji wenza na kama hiyo haitoshi Ujerumani ilionja chungu tena katika nusu fainali ya kombe la dunia nchini Afrika kusini mwaka 2010, wakati ilipokubali kipigo cha bao 1-0 pia dhidi ya Uhispania. Ujerumani iliridhika wakati huo kushika nafasi ya tatu. Kwa hivi sasa timu hizi zinaonekana kuwa katika kiwango sawa.
Timu ya taifa ya Ujerumani iliyo na wachezaji chipukizi zaidi, ilipigiwa upatu katika fainali za kombe la dunia mwaka 2010 kuwa ilisakata soka safi licha ya kuishia katika nafasi ya tatu.
Ujerumani na Hispania sawa
Miaka miwili baadaye wataalamu wanaziona timu hizi mbili zinazopigiwa upatu kulinyakua kombe la mataifa ya Ulaya kuwa ziko katika kiwango kinachofanana.Kwa kuwa Hispania kama Ujerumani ilishinda michezo yake yote ya kuwania kufuzu kucheza katika fainali hizi bila kushindwa na kuwa timu zinazoonekana kuweza kutoroka na taji hili mwaka 2012 nchini Poland na Ukraine. Huenda timu hizi zikapambana katika nusu fainali, ama katika fainali, iwapo zitafanikiwa kushika nafasi ya kwanza katika makundi yao ya awali.
Hispania ni timu bado yenye uwezo mkubwa , anasema hivyo kocha wa Ujerumani Joachim Löw. Lakini naona ishara kuwa timu za mataifa mengine zimesonga mbele. Katika hizo sisi pia tumo, amesema kocha Löw.
Kwa hilo hata mwenzake wa Hispania Vecente del Bosque analitambua. Ujerumani, amesema kocha huyo wa mabingwa wa dunia, imefanya kazi nzuri katika miaka ya hivi karibuni, sio tu katika kada ya timu iliyopo, lakini pia upande wa vijana chipukizi.
Löw katika timu ya taifa ameunda kikosi mahiri cha wachezaji wenye vipaji.
Wawili kati yao ni Mesut Özil na Sami Khedira ambao wamo katika kikosi cha mabingwa wapya wa Hispania , Real Madrid. Lakini pia hata ukilinganisha baina ya timu za Uhispania na Ujerumani hakuna tofauti kubwa.
Walinda mlango mahiri duniani
Kwa upande wa walinda mlango timu zote zina wachezaji mahiri kabisa. Uhispania ina Iker Casillas , mlinda mlango aliyechukua taji la kuwa namba moja mara tatu duniani. Manuel Neuer ni golikipa wa kisasa, akiwa na uwezo wa kuanzisha mashambulizi ya haraka kwa kurusha mipira , pamoja na uwezo wa kuzuwia jambo analolipendelea sana kocha Löw, kuhusu uanzishaji wa mashambulizi ya haraka kwa adui.
Sehemu inayovutia zaidi ya timu hizi mbili ni sehemu ya kiungo. Wakati nyota kutoka Barcelona , kina Andres Iniesta, Xavi na Cesc Fabregas, wakifanya vitu vyao, wakipigiana pasi fupi fupi zenye uhakika , si rahisi kuuondoa mpira miguuni mwao. Lakini hata wachezaji wa kiungo wa timu ya Ujerumani ni miongoni mwa wachezaji wa kiwango cha juu duniani.Mtaalamu Özil, Bastian Schweinsteiger na Khedira na pia Tony Kroos wana uwezo mkubwa wa kuwabana maadui na kuanzisha mashambulizi ya haraka langoni mwa adui. Hukaba adui haraka kuanzia katika eneo la ulinzi, na kusogea kwa kasi kubwa katika goli la adui.
Timu ngumu kama Hispania si rahisi kuishinda kwa mabavu ama ustadi wa kulinda lango, amekiri kocha wa Ujerumani Joachim Löw. Hispania unaweza kuishinda tu iwapo utacheza kwa mpangilio ulio mzuri.
Mwandishi : Nestler, Stefan / ZR/ Sekione Kitojo
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman