Ujerumani na Brazil zashindwa kukubaliana juu ya Iran
11 Machi 2010Katika mazungumzo na mwenyeji wake Waziri wa Nje wa Brazil Celso Amorim, mjini Brasilia, viongozi hao wa wili walishindwa kukubaliana juu ya suala la kuiwekea vikwazo Iran kuhusiana na mpango wake wa nyuklia wenye utata.
Waziri Amorim alimwambia Bwana Westerwelle kuwa Brazil haikubaliani na pendekezo la kuiwekea vikwazo zaidi Iran , na kwamba inataka kuona mzozo huo unamalizwa kwa njia za kidiplomasia zaidi.Hata hivyo walikubaliana kuwa ni muhimu kuzuia kuibuka kwa taifa jipya lenye nguvu za nyuklia.
Waziri huyo wa nje wa Brazil alisema kuwa kile kinachohitajika ni uwazi na ukweli kutoka jumuiya ya kimataifa kuhusiana na suala hilo, lakini pia hakusita kuitaka Iran kuwa tayari kuingia katika majadiliano.
Kwa upande wake Bwana Westerwelle alisema kuwa kuna tofauti kubwa aliyoiona katika kutathimini kitisho cha Iran, kwani kijiografia, umbali kati ya Brazil na Iran, na ule wa Ulaya na Brazil ni mkubwa, ambapo umbali kati ya Iran na Ulaya ni mdogo.Kwahivyo amesema bara hilo la Ulaya lina wasi wasi mkubwa na mpango huo wa nyuklia wa Iran.
Ameonya kuwa, bado wako tayari kwa mazungumzo, lakini kutokana na Iran kuonekana kushindwa kuupokea mkono wa kirafiki uliyonyoonshwa na Ulaya, basi hakuna budi kufikiria njia nyingine ya kuizuia.
Brazil imekuwa ikisita kukubaliana na azimio linalongozwa na Marekani la kutaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha duru ya nne ya vikwazo dhidi ya Iran.Iran imekuwa ikikanusha madai ya kutaka kutengeneza silaha za nyuklia na kusema kuwa mpango wake huo ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Azimio hilo linahitaji angalau kura nane, za wanachama wa Baraza la Usalama la umoja huo, na bila ya kura ya veto, ili lianze kutumika.Brazil haina kura ya veto, lakini kwa sasa ni moja kati ya wanachama 15 wa baraza hilo.
Ujerumani pamoja na mataifa matano yenye kura ya veto kwenye baraza hilo, kwa muda sasa zimekuwa zikiongoza juhudi za kutaka kuizuia Iran kuendelea na mpango wake huo wa nyuklia.
Mawaziri hao wa nje wa Ujerumani na Brazil, pia waliungana na jumuiya ya kimataifa kushutumu hatua ya Israel kuidhinisha ujenzi wa nyumba 1,600 za walowezi wa kiyahudi katika maeneo ya waarabu inayoyakalia kwa nguvu huko Jerusalem ya Mashariki.
Waziri wa Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle baadaye alikutana na Rais Luiz Inacio Lula da Silva mjini Sao Paulo ambapo mazungumzo yao yalituwama zaidi katika masuala ya amani duniani, mzozo wa kiuchumi uliyoikumba dunia pamoja na mabadiliko katika Umoja wa Mataifa.
Aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya mkutano huo kuwa Brazil ni nchi yenye ushawishi mkubwa duniani, kiasi kwamba inahitajika katika kukabiliana na vitisho vya usalama duniani.
Bwana Westerwelle anaongozana na ujumbe wa wafanyabiashara, ambao wanajaribu kutafuta mikataba mikubwa katika ujenzi wa reli pamoja na mitambo ya nishati ya jua nchini Brazil.
Waziri wa Maendeleo wa Brazil Miguel Jorge katika mkutano wake na Westerwell alisisita kuwa nchi yake inataka kushirikiana kwa karibu zaidi na Ujerumani katika maandalizi ya fainali za soka za dunia mwaka 2014, kwa kutumia teknolojia ya nishati ya jua kuimarisha viwanja vyake vya mpira.
Ujerumani ni ya mshirika wa nne kibiashara na Brazil, baada ya China, Marekani na Argentina.
Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP
Imepitiwa na:Oummilkher Hamidou