Ujerumani na Brazil 0:0/Nigeria na korea 0:0
6 Agosti 2008Waandazi wa michezo ya 29 ya olimpik inayofunguliwa rasmi ijumaa hii, wamearifu leo kwamba kila kitu sasa tayari kwa ufunguzi rasmi.
Mkurugenzi wa Kamati ya Maandalio ya Ufunguzi na kuifunga michezo hiyo Zhang Heping,amesema kwamba baada ya majaribio 3 sasa kila kitu kiko mahala pake.
Ingawa ufunguzi rasmi ni ijumaa, firimbi ililia leo kuanzisha dimba la wanawake la olimpik: Ujerumani mabingwa wa dunia, walitoka suluhu 0:0 na Brazil-makamo-bingwa wa dunia.
►◄
Kwa kweli, mpambano huu wa dimba wa ufunguzi ni kama finali yenyewe ya dimba la olimpik.Katika robo-saa ya kwanza Ujerumani ilikosa nafasi nzuri ya kulifumania lango la Brazil.Lakini hata Brazil mara 2 nusura itie bao. Kwanza mnamo dakika ya 4 ya mchezo pale kipa wa Ujerumani alipoutema mpira karibu na chaki ya lango lake. Halafu pale mchawi wa dimba wa Brazil Marta,alipouelekeza mkwaju mkali kutoka wingi wa shoto uliomstukia Christina lakini aliekosea kuusindikiza wavuni kwa kichwa.
Wasichana wa Ujerumani wakionesha nguvu zao za dimba na Sandra Viesek alikosea kidogo tu kutia bao la kwanza la Ujerumani mnamo dakika ya 24 ya mchezo. Birgit Prinz nae alikosa chupuchupu daika tu kabla firimbi ya mapumziko.Mastadi wa kiume wa Brazil akina Ronaldinho na Diego wako uwanjani kuwashangiria wenzao wakike . Brazil na Ujerumani ziliporudi uwanjani kwa kipindi cha pili ,Brazil ikicheza kwa kasi zaidi na Marta alikosa nafasi nzuri kabisa dakika 22 kabla ya firimbi ya mwisho kutia bao.
Ujerumani mnamo robo-saa ya mwisho ilileta wachezaji 2 wapya lakini hawakufua dafu.Kwa jumla, Brazil ilitamba zaidi,lakini haikuona mlango.
Nje ya uwanja wa dimba la Olimpik, mwenge wa olimpik uliokumbana na misukosuko njiani hasa katika nchi za magharibi, uliwasili jana Beijing tayari kwa msafara wake wa mwisho kabla kuwasili Uwanja mkuu wa olimpik wa "jumba la ndege" hapo ijumaa.
Mbio za kwenda na mwenge mjini Beijing, zitaanza leo huko "Forbidden City" kaskazini kidogo na uwanja maarufu wa Tianamen Square.
Msafara huo utadumu zaidi ya masaa 4 ukienda masafa jumla ya km 16.442.
Ujerumani imeshamteua nani atashika bendera ya Ujerumani siku ya ufunguzi pale kikosi chake kitakapoteremka uwanjani.Ni stadi wake wa mpira wa kikapu-"basketball" Dirk Nowitzki.
Mkuu wa timu ya wanariadha wa Ujerumani-chef de mission katika kijiji cha olimpik Michael Vesper alisema tumemchagua Nowitzki kwa kuwa hakuna mwengine anaewakilisha ndoto ya olimpik zaidi kama yeye."
Nowitzki anaecheza basketball kwa klabu ya Dallas Mavericks,Marekani,
ndie aliechangia mno kwa Ujerumani kufuzu kucheza katika olimpik.
Wakati ufunguzi rasmi ukinyemelea kumezuka visa vingi vya kisiasa:
Marekani imeilaslamikia serikali ya China kwa kukikatalia ruhusa ya kuiingia nchini kikundi cha wakereketwa wa Marekani kwa Dafur.
Isitoshe, raia 2 wa Marekani na 2 wa Uingereza, walitiwa leo kizuizini baada ya kufanya maandamano kuiungamkono Tibet karibu na Uwanja mkuu.
Katika kisa kingine,waendeshaji 4 wa mbio za baiskeli wa Marekani waliwasili kushiriki katika michezo hii ya Beijing wakivaa vifuniko vya pua kuvuta pumzi.Baadae wametaka radhi kwa kitendo chao hicho na hivyo kuipambazua hali ya hewa iliotishia kuchafua michezo ya Beijing.