1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuwa na serikali nyengine ya mseto

27 Septemba 2021

Chama cha siasa za mrengo wa kati kushoto, SPD, kinaongoza mbele ya muungano wa kihafidhina wa CDU/CSU kwa takribani asilimia 2, kwa mujibu wa matokeo yanayoendelea kutolewa kufuatia uchaguzi wa Jumapili.

https://p.dw.com/p/40uEk
Bundestagswahl | Wahlparty SPD | Olaf Scholz
Picha: Wolfgang Kumm/dpa/picture alliance

Kwenye matokeo haya ya awali, hadi sasa SPD ina asilimia 25.8 ya kura, ikiwa mbele kidogo ya chama cha siasa za mrengo wa kati kulia, CDU, na mshirika wake kutoka jimbo la Bavaria, CSU, ambavyo kwa pamoja vina asilimia 24.1.

Pande zote mbili, SDP na CDU/CSU, zimesema zinataka kuongoza serikali ijayo, na kimahesabu, upande wowote unaweza kufanya hivyo, endapo utapata washirika wanaohitajika kuunda serikali ya mseto.

Kwa upande wake, chama cha walinzi wa mazingira, Die Grüne, kinaonekana kuweka rikodi ya matokeo mazuri kabisa kuwahi kuyapata, kikiwa hadi sasa na asilimia 14 ya kura. Chama kinachopendelea wafanyabiashara cha FDP kina asilimia 11.5, ambapo kile cha siasa kali za mrengo wa kulia, AfD, kikiwa na asilimia 10.5. Chama cha siasa za mrengo wa kushoto, kina asilimia 5 kufikia sasa.

Matokeo haya ya awali yanaonesha kwamba vyama vinavyofuata siasa za mrengo wa kati kushoto ndivyo vilivyopata ushindi mkubwa kabisa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Vyote viwili, yaani SPD na Die Grüne, vinaelekea kupata ongezeko la asilimia 5 zaidi inapolinganishwa na matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2017.

Kinyume chake ni muungano wa kihafidhina wa CDU/CSU ambao ndio uliopoteza zaidi kwenye uchaguzi huu wakati kiongozi wake wa muda mrefu, Angela Merkel, akihitimisha zama zake. Ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2017, muungano huo umeanguka kwa asilimia 8, yakiwa matokeoa mabaya kabisa tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia.

Uwezekano wa serikali mpya ya muungano wa vyama

Bundestagswahl - Wahlparty CDU/CSU | Armin Laschet
Mgombea ukansela kupitia muungano wa CDU/CSU, Armin Laschet, yuko nyuma ya mgombea wa chama cha SPD, Olaf Scholz.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Suali kubwa linaloulizwa ni ikiwa matokeo haya yatakuwa na maana gani kwa serikali ijayo? 

La kwanza, ni kwamba kutokana na mchuano ulivyo mkali, uwezekano wa serikali ipi ya mseto itakuwepo bado hauko wazi. 

Kwa mujibu wa makisio haya ya awali, uwezekano moja ni kuendelea kwa kile kiitwacho "mseto mkubwa", ama grandkoalition kwa Kijerumani, wa muungano wa CDU/CSU na SPD, ambao umekuwepo Ujerumani tangu mwaka 2013.

Hata hivyo, kwa kuwa vyama vyote viwili vikubwa kabsia vinataka kuongoza serikali ijayo, Ujerumani inaweza kujikuta ikielekea kwenye kile kiitwacho "mseto wa njia tatu" kwa mara ya kwanza tangu miaka ya 1960 katika kiwango cha serikali kuu ya shirikisho.

Hiyo inaweza kumaanisha serikali ya mseto ya vyama vya CDU/CSU pamoja na Die Grüne na FDP. Ama SPD kuunda mseto huo na Die Grüne na FDP.

Hakuna chama hata kimoja ambacho kimekubali kuingia kwenye muungano na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, AfD, na ambacho, kwa hivyo, kina uhakika wa kusalia kuwa chama cha upinzani.

Merkel kuendelea kuwa kiongozi wa mpito

Bundestagswahl 2021 | Wahlparty der CDU
Kansela Angela Merkel (kushoto) na Armin Laschet.Picha: Martin Meissner/AP/picture alliance

Kuchaguliwa kwa kansela mpya kwenye bunge la Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, ama Bundestag, hakutafanyika hadi serikali mpya ya mseto iwe imeundwa. Jambo hilo linaweza kuchukuwa hata wiki kadhaa kama sio miezi.

Lakini mgombea wa nafasi ya ukansela kupitia SPD, Olaf Scholz, amesema ana mategemeo kuwa mazungumzo ya uundaji wa serikali ya mseto yatakuwa yamekamilika kufikia Krismasi. 

Kauli kama hiyo imetolewa pia na mgombea mwenzake wa ukansela kutokea CDU, Armin Laschet, ambaye naye anataka serikali iwe imeundwa kabla ya Krismasi. 

Wakati hilo likisubiriwa, Kansela Angela Merkel ataendelea kuwa madarakani kwa nafasi ya kiongozi wa mpito. 

Yaliyovuma kwenye uchaguzi

Miongoni mwa matukio yaliyovuma kutokana na uchaguzi wa mwaka huu ni lile la kusini mwa Ujerumani katika jimbo la Bavaria, ambako mtu aliyejibadilisha jinsia alielekea kuchaguliwa kuwa mbunge katika bunge la shirikisho, Bundestag.

Bundestagswahl | Wahlparty FDP
Viongozi wa chama cha kiliberali cha FDP, ambacho kinashika nafasi ya nne.Picha: Sebastian Kahnert/dpa/picture alliance

Tessa Ganserer, ambaye amekuwa mjumbe wa bunge la jimbo la Bavaria tangu mwaka 2013, aligombea kiti hicho kwa tiketi ya chama cha Kijani, ama die Grüne, na kupata asilimia 22.6 katika kura ya kwanza.

Tukio jengine ni la chama cha CDU cha Kansela Merkel kupoteza kiti cha ubunge katika eneo analotokea kansela huyo, ikiwa ni mara ya kwanza ndani ya miongo mitatu, na kiti hicho sasa kimemwendea mgombea hasimu cha SPD.

Hii ni mara ya kwanza kiti hicho kumwendea mbunge wa chama chengine kisichokuwa CDU tangu mwaka 1990.

Merkel alishinda kiti hicho katika jimbo hilo la Vorpommern-Rügen katika uchaguzi wa kwanza huru baada ya Ujerumani Mashariki na Magharibi kuungana na akakitetea katika chaguzi saba mfululizo.