Ujerumani kurekebisha masaibu yake dhidi ya Uholanzi
19 Novemba 2018Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew amesema jana Jumapili kuwa kiwango cha kukatisha tamaa kilichooneshwa na timu ya taifa katika mwaka 2018 kinakatisha tamaa na sasa kinalenga katika kile mabingwa hao wa zamani wa kombe la dunia wanahitajika kufanya ili kurejea katika hali yake ya kawaida.
Ujerumani inakwaana na Uholanzi leo Jumatatu katika mchezo wao wa mwisho wa ligi ya mataifa , ambapo tayari wamekwisha shuka daraja, na wanajaribu tu kunusuru mwaka ambao umekuwa na matatizo makubwa kwa kikosi hicho kwa kucheza vizuri leo jioni.
Waliuanza mwaka huu wa 2018 wakiwa mabingwa watetezi na timu iliyopigiwa upatu kurejesha kombe la dunia nyumbani nchini Urusi, lakini waliondoka katika michuano hiyo mapema katika muda wa miaka 80 na timu hiyo inaelekea katika mwaka 2019 ikiwa imefungwa mara sita hadi sasa katika mwaka mmoja. Mchezaji wa ulinzi wa Die Mannschaft Joshua Kimmich amesema kuporomoka daraja ni lazima tukuweke mbali na tuanze upya.
"Ndio, hali ya kushuka kutoka kundi la ligi ya mataifa, ni lazima tusahau. Ni wazi kwamba kwetu kesho ni mchezo usio na umuhimu, lakini tutauchukulia kwa dhati na pia tunataka kushinda bila kujali ukweli kwamba tuko wa mwisho katika kundi. Bila shaka tunataka kumaliza mwaka huu, ambao ulikuwa mbaya, kwa mchezo mzuri."
Mwaka wa kukatisha tamaa
Pigo la mwisho kwa kikosi cha Joachim Loew lilikuja siku ya Ijumaa wakati kikosi cha Uholanzi kilipoishinda Ufaransa na kuhakikisha kwamba Ujerumani inashuka daraja katika mashindano hayo mapya ya ligi ya mataifa. Kocha Joachim Loew alikuwa na haya ya kusema.
"Inasikitisha kwetu , bila shaka, kwa mchezo wa kesho, kwamba hatuwezi kubadili chochote hivi sasa inapokuja katika ligi ya mataifa. Wiki iliyopita, nilisema kwamba ninapaswa kukubali kwamba mwaka huu ulikuwa wa kukatisha tamaa sana, kwamba tunajifunza mambo muhimu na tunachukua hatua sahihi kwa ajili ya mwaka ujao na mwaka 2019 na hapo baadae na katika michuano ya mwaka 2020."
Lakini kuna matumaini ya hapo baadaye kwa kuijenga upya timu ya taifa ya Ujerumani kutokana na vijana chipukizi kama zilivyo timu nyingine za taifa. Loew alimwacha mlinzi wa kati Jerome Boateng katika michezo miwili na kuwaacha katika benchi wachezaji wengine wawili wazoefu Thomas Mueller na Mats Hummels. Leo huenda kikosi hicho kikacheza bila mchezaji wa pembeni Marco Reus, ambaye ana maumivu madogo ambayo yamesababisha pia kutocheza dhidi ya Urusi. Loew tena.
"Ni kipi kingine kinaweza kuwa muhimu , ni mchezo hapo kesho kwa ajili ya kuingia katika chungu sahihi cha kupangwa katika makundi kwasababu timu 10 za kwanza katika kundi A zinatoka katika chungu cha kwanza. Kwa hiyo Iceland iko nyuma yetu, Poland ina pointi moja, sisi tuna pointi moja, kwa hiyo matokeo ni muhimu kwetu ili tuwe katika chunga namba moja Desemba 2. Sababu nyingine muhimu ni kama nilivyosema, tunataka kuuaga mwaka huu vizuri, kwa mchezo mzuri. Kwetu sisi, na bila shaka kwa mashabiki wetu, pia kuonesha tuko katika njia sahihi ya kufufuka."
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / ape / afpe / rtre
Mhariri: Yusuf , Saumu