Ujerumani kupimana ubavu na Italia
14 Novemba 2016Ikiwa bado inakabana na Uhispania kwa kuwa na pointi sawa katika kundi G, Italia itarejea katika mfumo wake wa kawaida wa 3-5-2 kwa mchezo wa kesho dhid ya Ujerunani baada ya kuamua kutumia mfumo wa 4-2-4 na kuikandamiza Liechtenstein kwa mabao 4-0 siku ya Jumamosi.
Hata hivyo matumaini ya ushindi kwa vijana wa Joachim Loew , ambao walishinda mchezo wa kirafiki Machi mwaka huu kwa mabao 4-1 mjini Munich kabla ya kuishinda Italia tena kwa mikwaju ya penalti katika robo fainali ya Euro 2016 katikati ya mwaka huu , yatakuwa juu.
Loew , ambaye aliweka rekodi mpya ya kufikisha ushindi wa michezo 95 akiwa na timu ya taifa ya Ujerumani wakati Die Mannschaft ilipoishindilia San Marino kwa mabao 8-0 siku ya Ijumaa, inatarajiwa kutumia mchezo huo kufanya majaribio wakati jicho likiwa katika kombe la mabara la dunia la Confederation. baada ya ushindi huo ambapo mchezaji chipukizi Serge Gnabry alipachika mabao matatu, mchezaji wa kati kutoka Manchester City Ilkay Gundogan alikuwa na haya ya kusema.
"Ni wazi kwamba kwa sasa hakuna kipimo maalum kwetu. Pamoja na hayo ilikuwa muhimu kuweka mwendelezo uwezo wa mchezo wetu. Kwa kupata mabao mawili ya mapema, hali ilikuwa nzuri. Haikuwa rahisi hata hivyo, dhidi ya watu kumi, ambao wako katika ulinzi, hilo pia lilikuwa wazi. Hatimaye tulishinda kwa mabao 8-0. Kwa hiyo kila kitu kiko sawa na mambo yanaendelea."
Mchezaji wa kati wa Juventus Turin Sami Khedira na mchezaji wa kati wa Arsenal Mesut Ozil wote watapumzishwa, ikiwa na maana kwamba huenda mchezaji wa Wolfsburg Yannick Gerhart atapewa nafasi ya kucheza kwa mara ya kwanza katika kikosi hicho.
Wakati mlinda mlango wa kawaida manuel Neuer akiwa nje kutokana na homa, Bernd Leno wa Bayer Leverkusen atapewa wajibu wa kuwazuwia washambuliaji wa Squadra Azzuri wasifanye kile wanachokifanya kila mara dhidi ya Die Mannschaft.
Leo kikosi hicho cha Die Mannschaft kilikutana na kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis mjini Vatican kabla ya kuanza matayarisho ya mchezo huo wa kirafiki dhidi ya Italia.
Thomas Mueller na Mats Hummels wa Bayern Munich walimkabidhi Papa Francis jezi ya Ujerumani iliyotiwa saini na wachezaji wa kikosi hicho na kitambaa kilichochorwa na watoto kutokana na wakfu ulioanzishwa na mlinda mlango wa timu hiyo manuel Neuer.
Pope ambaye ni shabiki mkubwa wa kandanda ambaye timu ya nyumbani kwao Argentina ilipoteza mchezo wa fainali ya kombe la dunia mwaka 2014 dhidi ya Ujerumani , alisifu ujasiri wa timu ya taifa ya Ujerumani.
"Niliwahi mara nyingi kusikia kwamba ushindi wenu ni ushindi wa timu," alisema papa Francis akitambua kwamba timu hiyo inafahamika kama Die Mannschaft, yaani kikosi.
Mwandishi: Sekione Kitojo
Mhariri: Yusuf Samu