Ujerumani kuongeza ulinzi Mediterania
22 Juni 2016Taarifa kutoka kwa msemaji wa serikali imesema maamuzi hayo yamefikiwa baada ya Umoja wa Ulaya kulipa jeshi lake la majini mamlaka ya kukagua meli zitakazotiliwa shaka ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Operesheni Sophia, ambayo pia inalenga kuvunja makundi haramu yanayojihusisha na usafirishaji wa wahamiaji kwenda Ulaya.
Bunge la Ujerumani, Bundestag, linatarajia kuupitisha mpango huo kabla ya kuanza shughuli zake wakati wa majira ya joto, mwishoni mwa mwezi huu kimesema chanzo cha habari. Mamlaka hiyo ya jeshi pia itahusisha shughuli ya kuisaidia Libya kuboresha ulinzi kwenye ukanda wake wa pwani na jeshi lake la majini.
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Ursula von der Leyen, amesikika akielezea kuridhishwa na mpango huo, ulio chini ya azimio la Baraza la Umoja wa Mataifa la kupambana na uuzwaji haramu wa silaha, lililopitishwa wiki chache zilizopita.
Hivi ndivyo namna Ujerumani ilivyoshiriki katika mpango huo wa Umoja wa Ulaya kwa kutumia meli zake. Taarifa ya jeshi la Ujerumani inasema kiasi ya wanajeshi wake 950 wamesaidia kuwaokoa takriban wahamiaji 1,500 wanaosafiri kwa kutumia bahari tangu mwaka 2015.
Baada ya mpango huo kuridhiwa na bunge, meli za Ujerumani zitakuwa na uwezo wa kusimamisha, kukagua na kuzikamata manuwari zinazotumiwa na makundi hayo haramu yanayosafirisha wahamiaji, lakini pia kuwatia kizuizini watuhumiwa.
Jeshi hilo la Ujerumani pia litakuwa na mamlaka ya kukagua meli zinazoelekea na kutoka nchini Libya katika matukio yatakayohisiwa kuhusiana na uuzwaji haramu wa silaha.
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, mara zote amesisitiza umuhimu wa kuboresha hali ya mambo kwenye nchi kama Libya kama sehemu ya kumaliza mzozo wa wahamiaji unaolikabili bara la Ulaya.
Mwandishi: Lilian Mtono/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef