Ujerumani kukipiga na Uhispania ligi ya Mataifa Ulaya
31 Agosti 2020Baada ya mapumziko ya zaidi ya miezi tisa , kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani kikiongozwa na kocha Joachim Loew , na vikosi vingine vya kimataifa barani Ulaya , vinarejea uwanjani katika kinyang'anyiro cha Ligi ya mataifa. Athari za janga la virusi vya corona bado linatikisa na michezo hiyo itachezwa bila ya mashabiki kuwapo uwanjani.
Kiasi ya siku 286 zimepita baada ya kuipiga mweleka Ireland ya kaskazini kwa mabao 6-1, Joachim Loew anakusanya kikosi chake tena leo. Die Manschaft itafanya matayarisho yake mjini Stuttgart kwa muda wa siku chache tu kwa ajili ya pambano la Alhamis la Ligi ya Mataifa dhidi ya Uhispania kabla ya kwenda Basel ambako kikosi hicho kitakutana na miamba wa Uswisi siku ya Jumapili. Mashujaa walionyakua mataji matatu msimu huu wa Bayern Munich Manuel Neuer, Joshua Kimmich, Leon Goeretzka na Serge Gnabry wamepumzishwa.
Italia ambayo inaonekana kuimarika tena ni wenyeji wa Bosnia siku ya Ijumaa, na Uingereza inafanya ziara Iceland siku ya Jumamosi. Mabingwa wa dunia Ufaransa pia wanasafiri kwenda Sweden.
Kai Havertz
Kocha wa Bayer Leverkusen Peter Bosz anaitayarisha timu yake kwa ajili ya michezo ya Bundesliga msimu ujao bila kufikiria kuhusu mchezaji wa kati Kai Havertz na mshambuliaji Kevin Volland , na kwamba huenda wakakamilisha uhamisho wao hivi karibuni. Havertz anahusishwa na kuhamia Chelsea na Volland yuko njiani kuelekea Monaco nchini Ufaransa. "Natarajia kuwa hatarejea," Bosz alisema leo kuhusu Havertz , ambaye anajiunga na kikosi cha JoachimLoew katika timu ya taifa.
Vilabu 39 vya madaraja ya juu mawili nchini Ujerumani vinakutana kwa mkutano kwa njia ya vidio siku ya Alhamis kuendeleza majadiliano kuhusiana na kuwarejesha mashabiki uwanjani. Hakutakuwa na suluhisho la haraka ambapo viwanja vitupu vinatarajiwa kuendelea kuwa tupu hadi kiasi mwishoni mwa mwezi Oktoba baada ya uamuzi kupitishwa wiki iliyopita na kansela wa Ujerumani Angela Merkel pamoja na mawaziri wakuu wa majimbo kuendelea na marufuku dhidi ya mikusanyiko mikubwa.
Kundi la kikazi la kisiasa linaangalia nafsi kadhaa wakati taasisi inayoendesha ligi ya kandanda nchini Ujerumani DFL, imetoa wito wa suluhisho la uwajibikaji hatua kwa hatua ikitegemea na hali ya janga hilo", huenda kuanzia mwezi Novemba.
Timu ya wanawake ya Wolfsburg huenda imepoteza mchezo wake wa fainali ya Champions League dhidi ya Olympique Lyon jana Jumapili lakini mabingwa hao wa Bundesliga na kombe la shirikisho wanapigiwa upatu kutawala soka la wanawake tena nyumbani msimu huu. Wanaanza ligi wakipambana na Essen siku ya Ijumaa katika mchezo ambao ni kama marudio ya mchezo wa fainali ya kombe la shirikisho msimu uliopita.