Ujerumani kukabiliana na Austria kombe la dunia
10 Septemba 2012Mashindano ya olimpiki ya watu wenye ulemavu, Paralympics , mashindano yaliyomalizika rasmi Jumapili (09.09.2012) mjini London, yalikuwa ni tamasha la kusisimua na kufungwa kwa mashindano hayo kulifanyika kwa mara nyingine tena kwa mafanikio makubwa, baada ya siku 12 za michezo kadha iliyofanyika. Watayarishaji wa mashindano hayo ya mjini London waliahidi mashindano makubwa , katika historia ya miaka 52 ya michezo hiyo. Jumla ya wanariadha 4,200 walishindana katika michezo 503 katika viwanja karibu 20 vya watu wenye ulemavu. Walikuwa wakiwania medali 1,522 katika siku hizo 11 za mashindano.
Rais wa kamati ya kimataifa ya Paralympics Philip Craven ameasifu mashindano hayo kwa kusema yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
"Mashindano haya yamekuwa ya kushangaza na bila shaka kwa fikira zangu na zile za wanamichezo walioshiriki , haya ni mashindano makubwa kabisa ya paralympics kuwahi kufanyika hadi sasa".
Nae mwanariadha maarufu kutoka Afrika kusini Oscar Pistorius ambaye alivuliwa taji la ubingwa wa mita 200, lakini akanyakua ubingwa wa mbio za mita 400, alikuwa kivutio kikubwa katika mashindano haya na pia mashindano ya kawaida ya olimpiki.
Oscar Pistorius akitathmini mashindano haya amesema na hapa namnukuu.
"Nafikiri watu wengi zaidi duniani wameangalia mashindano haya ya Paralympics. ilikuwa ni rahisi zaidi kuweza kuyaona. London ni moja kati ya miji iliyofanikiwa zaidi duniani katika mashindano ya olimpiki na watu duniani kote waliweza kutathmini, sio tu kuona michezo ya wenye ulemavu, lakini waliona michezo na wanamichezo ambao walikuwa wana ulemavu kwa mara ya kwanza . Nafikiri hiki ni kitu cha kufurahisha zaidi. Dhana zinabadilika na ni kutokana na kila mtu aliyehusika".
Meya wa jiji la Rio De Janeiro nchini Brazil amekabidhiwa bendera ya michezo hii ya Paralympics. Mji huo wa Brazil , utakuwa mwenyeji wa mashindano ya olimpiki na paralimpiki katika mwaka 2016.
Soka.
Ujerumani inaingia uwanjani kesho Jumanne kukwaana na Austria katika mchezo wake wa pili katika juhudi za kuwania tikiti ya kucheza katika fainalia za kombe la dunia , nchini Brazil mwaka 2014. Yanatarajiwa mabadiliko katika kikosi cha kocha Joachim Loew, kutoka kile kilichoingia uwanjani kupambana na visiwa vya Faroar mjini Hannover Ijumaa iliyopita, ambapo Ujerumani iliibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 3-0. Mabadiliko hayo yanaonekana kuwapo katika sehemu ya kiungo ambapo Ujerumani inatarajiwa kucheza na wachezaji wawili wa kiungo katika ulinzi, ambapo Sami Khedira atasaidiwa na Toni Kroos.
Hata hivyo Austria inaingia katika kampeni hii ya kombe la dunia mwaka 2014 kwa matumaini mapya ,kutokana na kizazi kipya cha wachezaji na wengi wao wanacheza soka katika bundesliga. Ujerumani pia inaonekana kuwa dhaifu kidogo baada ya kufanya vibaya katika mashindano ya kombe la Euro 2012 baada ya kutolewa na Italia kwa mabao 2-1 katika nusu fainali ya mashindano hayo.
Kocha Marcel Koller raia wa Uswisi atakuwa kwa mara ya kwanza katika benchi la ufundi akiongoza kikosi cha Austria dhidi ya Ujerumani.
Baada ya kufanya vibaya katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Bulgaria Ijumaa iliyopita , Itali inamatumaini ya kupata ushindi dhidi ya Malta mjini Modena kesho.
kikosi cha Cesare Prandeli kilitosheka na sare ya mabao 2-2 mjini Sofia dhidi ya Bulgaria.
Uingereza itabidi kuridhika kuwakosa wachezaji sita muhimu wa kikosi cha kwanza wakati ikijaribu kujenga mwanzo mzuri katika kampeni yake katika kundi H la dhidi ya Ukraine kesho Jumanne.
Ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya moldova umekuja kwa gharama kubwa ya kumkosa mlinzi John Terry akijiunga na mchezaji mwenzake wa Chelsea Ashley Cole katika orodha ya majeruhi, pamoja na Wayne Rooney, Andy Carroll, Gareth Barry , Ashley Young na Scott Parker.
Uholanzi inamiadi na Hungary hapo kesho Jumanne. Uhispania inaanza safari ndefu ya kutetea taji lake la ubingwa wa dunia kwa safari ya kwenda Georgia , wakati Ufaransa na Ureno zina nafasi ya kufikisha points sita katika michezo miwili iwapo zitapata ushindi.
Ufaransa inawaalika Belarus katika kundi I, na Ureno ya Cristiano Ronaldo ina kibarua na Azerbaijan katika kundi F.
Ubelgiji itaonyeshana kazi na Croatia , timu zote hizo zilianza kampeni hii kwa ushindi , Wabelgiji wakiishnda Wales kwa mabao 2-0 na Croatia wakiwashinda nguvu Macedonia.
Tennis.
Victoria Azarenka amemsifu bingwa wa US open kwa upande wa wanawake Serena Williams kuwa ni mchezaji bora kabisa na kuahidi kujifunza kutokana na kushindwa kwake mara ya kumi katika mapambano yao 11 waliyokwisha kutana.
Williams amenyakua taji la nne la US Open mjini New York jana jumapili na kufikisha mataji 15 katika muda wake akiwa mchezaji kwa ushindi wa seti mbili kwa moja, kwa 6-2, 2-6 na 7-5 , ikiwa ni fainali ya kwanza ya wanawake kwenda umbali huo katika muda wa miaka 17.
Na huko mjini Nairobi Kenya yanafanyika mashindano ya bara la Afrika ya kuogelea katika uwanja wa kimataifa wa Moi mjini Nairobi.Tanzania haikupeleka wachezaji wake katika mashindano hayo, kutokana na matatizo ya fedha yanayokikumba chama hicho. Amesema hayo katibu mkuu wa chama cha waogeleaji nchini Tanzania, TSA , Noel Kiunsi.
Kwa taarifa hiyo basi mpenzi msikilizaji ndio sina budi kusema tumefikia mwisho wa kuwaletea habari hizi za michezo, hadi mara nyingine jina langu ni Sekione Kitojo , kwaherini.
Mwandishi : Sekione Kitojo /afpe / dpae/ rtre
Mhariri. Mohammed Abdul Rahman