Ujerumani kuipatia Ugiriki Euro bilioni 22.4
3 Mei 2010Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema kuwa nchi yake itatoa kiasi cha Euro bilioni 22.4 kama sehemu ya mpango wa kuinusuru Ugiriki, kwa kuipatia mkopo ili iondokane na mzozo wake wa madeni, ambapo amesema mkopo huo utakuwa wenye manufaa. Akizungumza na waandishi habari kwenye mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, Kansela Angela Merkel amesema kuwa fedha hizo zitaisaidia Ugiriki na pia zitadhibiti sarafu ya Euro kwa ujumla na hivyo kuwasaidia wananchi wa Ujerumani. Bibi Merkel ametoa tangazo hilo baada ya baraza lake la mawaziri leo kupitisha kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kuinusuru Ugiriki kabla ya mkutano wa viongozi wa taifa na serikali wa kundi la nchi zinazotumia sarafu ya Euro mwishoni mwa wiki hii.
Mpango huo wa Ujerumani kuipatia mkopo Ugiriki sasa utatakiwa kufikishwa bungeni kwa ajili ya kuidhinishwa na bunge la nchi hiyo-Bundestag, siku ya Ijumaa. Mpango huo wa kuipatia Ugiriki mkopo utakuwa katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ambapo jumla ya Euro bilioni 110 zitatolewa na kundi la nchi zinazotumia sarafu ya Euro.Hatua ya baraza la mawaziri la Ujerumani kupitisha kiasi hicho cha fedha imefikiwa baada ya serikali za Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF jana Jumapili kukubaliana kutoa mkopo wa Euro bilioni 110 kwa ajili ya kuinusuru Ugiriki isifilisike.
Hata hivyo, chama cha upinzani nchini Ujerumani Social Democrats-SPD, kimesema kitaunga mkono mpango huo wa kuinusuru Ugiriki, iwapo tu Kansela Angela Merkel atajizatiti zaidi katika kuyahusisha kwa kiwango kikubwa mabenki. Joachim Poss, makamu mwenyekiti wa wabunge wa SPD, amesema chama chake kitaamua iwapo kiunge mkono mpango huo baada ya kushauriana na serikali, lakini Kansela Merkel anatakiwa kutia msukumo zaidi kwa kodi ya Ulaya na kuweka kikomo cha ushawishi wa walanguzi wa masoko.
Nchini Ugiriki kwenyewe
Wakati hayo yakijiri, nchini Ugiriki kwenyewe, vyombo vya habari nchini humo vimeonya kuwa nchi hiyo inakabiliwa na enzi mpya ya mateso baada ya serikali ya Ugiriki kutangaza hatua ya kupunguza matumizi yake na kuongeza kodi kama sehemu ya mpango wa kupata mkopo kutoka kwa nchi za Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF. Katika uhariri wake, gazeti la Ta Nea linaloiunga mkono serikali limeandika kuwa hali ya maisha ya wananchi wa Ugiriki imebadilika tangu jana.
Gazeti hilo limeandika kuwa mpango huo mpya umezikumba sekta zote za umma na kwamba hatua hiyo ya kukabiliana na mzozo wa madeni unaathiri maisha ya wananchi. Ili kupunguza matumizi ya Euro bilioni 30, kutoka kwenye bajeti ya serikali kwa miaka mitatu, serikali ya Ugiriki inatakiwa kupunguza mishahara ya wafanyakazi wa sekta ya umma, kupunguza malipo ya uzeeni, kuongeza kodi na muda wa kustaafu.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE/APE/RTRE)
Mhariri: Abdul-Rahman