1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuachana na nyuklia kuna maana gani?

1 Julai 2011

Serikali ya Ujerumani imebadilisha muelekeo wake kuelekea nishati kwa kuachana na nyuklia, ambapo sasa taifa hili la nne kiuchumi duniani limeamua kutumia nishati jadidifu ili kulinda usalama wake na mazingira.

https://p.dw.com/p/11nDu
Chansela Angela Merkel wa Ujerumani
Chansela Angela Merkel wa UjerumaniPicha: DW

Hatua kwa hatua, Chansela Angela Merkel anashirikiana na Mkuu wa Shirika la Ulinzi wa Mazingira, Greenpeace, Kumi Naidoo, katika mapambano ya kuifanya dunia iishi bila ya mitambo ya nyuklia, bali iishi ikiwa ni mitambo tele ya kuzalishia umeme kwa nishati za upepo, jua na ile inayotokana na viumbe vyenye uhai.

Kwa mwezi mzima uliopita, hilo lilikuwa ni wazo lililokuwa likiwasilishwa kwenye katuni za magazetini, ila hatimaye umekuwa ukweli ambao Bunge la Ujerumani hapo Alkhamis (30.06.2011) liliamua kuukabili.

Sasa nishati jadidifu ndizo zitakazokuwa chanzo cha umeme wa taifa hili la nne kwa uchumi mkubwa duniani na wakati huo huo njia ya kuyanusuru mazingira duniani.

Uamuzi huu ni jibu la Ujerumani kwa maafa ya Fukushima ambalo huko nje linaweza kuchukuliwa na kuonekana kama tabia halisi ya "Woga wa Kijerumani".

Mabango yanayosomeka "Funga Vinu vya Nyuklia" mbele ya bunge la Ujerumani
Mabango yanayosomeka "Funga Vinu vya Nyuklia" mbele ya bunge la UjerumaniPicha: picture alliance/dpa

Inaweza ikaonekana rahisi hivyo, hasa kwa sababu ya raia wa Ujerumani kuikataa nishati ya nyuklia. Lakini pia kuna sababu nyengine muhimu zaidi: nayo ni hasara za uzalishaji wa umeme wa nyuklia. Nishati hii si ya kudumu na inapingwa duniani kote na teknolojia ya mazingira.

Uamuzi kwamba ifikapo mwaka 2020, vinu vya nyuklia vitakuwa vimeshafungwa kabisa, ni muelekeo unaokisika na ukweli halisi nchini Ujerumani.

Kilichofanywa na maafa ya Fukushima, ni kumpa Chansela wa Atomiki, Angela Merkel, uwezekano tu wa kuharakisha hatua hiyo na pia kuweka njia mbadala za kupatia nishati.

Kutakuwa ni kutia chumvi mno kudhani kwamba kwa Ujerumani kusema "hapana kwa vinu vya nyuklia" peke yake kunaweza kuubadilisha ufahamu wa ulimwengu kwa teknolojia hii ya hatari.

Wachina, Wahindi au Warusi hawatarajiwi kuacha kuacha ujenzi wa vinu vyao vya nyuklia, ati kwa sababu tu Ujerumani imefanya hivyo.

Labda mataifa haya yataweza tu kuamua jhivyo, baada ya kupambana na gharama halisi za nishati ya nyuklia, ikiwemo uwezekano wa maafa na pale itakapofikia mionzi inapenya kwenye vinu vyao na hawawezi tena kuizuia.

Ujerumani itakuwa kama jaribio la namna ambavyo uchumi unaweza kuendeshwa sio tu bila ya madini ya yuraniamu, bali pia kwa kiwango kidogo cha mafuta, gesi na au makaa ya mawe.

Kwa wale ambao watataka kuamua baadaye, Ujerumani itakuwa kama kigezo au kama teknolojia ya kufuatwa.

Kwa vyovyote vile, hakuna anayeweza kupuuzia ukweli kwamba Ujerumani imechukua uamuzi mgumu wa kuwa "mtangulizi" katika kubadilisha sera yake ya nishati.

Na kuhusu nchi zinazoinukia kiuchumi, mfano huu una maana pia. Tayari Chansela Merkel ameliweka bara la Afrika katika makini yake, kwa kufanya kazi na Mkuu wa Shirika la Ulinzi wa Mazingira la Greenpeace anayetokea Afrika ya Kusini, Kumi Naidoo: wote wawili wana dhamira ya kuliona bara hilo likiwa halina vinu vya nyuklia, maana halivihitaji; kwani kwenye bara hilo halina ukame wa jua, upepo, joto la chini ya ardhi na gesi ya viumbe vyenye uhai.

Mwandishi: Bernd Gräaßler/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Othman Miraji