1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani itaanzisha sheria ya kudhibiti uuzaji silaha

27 Desemba 2021

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema serikali mpya ya mseto itaanzisha sheria mpya ya kudhibiti uuzaji wa silaha nje ya nchi.

https://p.dw.com/p/44rXj
Deutschland Berlin | Annalena Baerbock, Außenministerin zu Afghanistan
Picha: Michael Sohn/AP Photo/picture alliance

Kauli hii inajiri baada ya kugundulika kwamba siku chache kabla ya kufikia mwisho utawala wa kansela wa zamani Angela Merkel uliidhinisha mauzo ya silaha ya karibu euro bilioni 5. 

Mwanasiasa huyo wa chama cha Kijani alitoa maoni hayo siku chache baada ya kufichuliwa kuwa utawala wa Kansela wa wakati huo Angela Merkel uliidhinisha mikataba ya mauzo ya nje yenye thamani ya karibu Euro bilioni 5 na mataifa ya Misri na Singapore wakati ikijiandaa kukabidhi madaraka.

Serikali mpya ya mseto inayoundwa na chama  cha Social Democrats (SPD), Chama cha Kijani na chama cha  FDP kinachotetea maslahi ya biashara, iliapa katika makubaliano ya muungano wao kudhibiti mauzo ya silaha kwa mataifa yanayoinukia yaliyo nje ya Umoja wa Ulaya na NATO. Hiyo itajumuisha Misri, ambayo imekuwa mmoja wa wanunuzi wakuu wa silaha za Ujerumani.

soma Annalena Baerbock mgombea ukansela wa chama cha Kijani

Serikali iliyopita iliidhinisha mauzo ya meli tatu za kivita na mifumo 16 ya ulinzi wa anga kutoka kwa kampuni ya Thyssenkrupp  na Diehl Defense kuelekea katika taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika. Uidhinishaji huo ulifanyika siku tisa za mwisho za utawala wa Merkel licha ya Misri kukosolewa juu ya rekodi ya haki za binadamu na kuhusika katika migogoro nchini Yemen na Libya.

Rikodi ya mauzo ya silaha

Ägyptisches U-Boot Typ 209/1400mod S 44
Picha: Joerg Waterstraat/SULUPRESS.DE/picture alliance

Vile vile mkataba wa kupeleka manowari ya kijeshi Singapore pia ulitiwa saini. Hata hivyo mtaalamu wa sera za kigeni kutoka kambi ya kihafidhina, Roderich Kiesewetter, alitetea mikataba hiyo ya serikali iliyoondoka, akisema ilifanywa "ndani ya mfumo halali wa kisheria."

Kiesewetter ameliambia shirika la habari la dpa kwamba ukosoaji kutoka kwa vyama vya mrengo wa kushoto "si chochote zaidi ya machozi ya mamba." na kusema kwamba ni muhimu kulinda maslahi ya usalama ya Ujerumani katika mageuzi yanayokuja ya udhibiti wa usafirishaji wa silaha.

Mikataba hiyo ilifanya mauzo ya silaha za Ujerumani kufikia rekodi mpya mnamo 2021 yenye thamani ya Euro bilioni 9.04. Rekodi ya awali ya mauzo ya silaha ya Ujerumani ilikuwa Euro bilioni 8.02 mwaka wa 2019 kabla ya janga la COVID-19.

Kulingana na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm, Ujerumani ni mojawapo ya wauzaji wakubwa wa silaha duniani pamoja na Marekani, Urusi na Ufaransa. Na ilihusika na asilimia 5.5 ya mauzo ya silaha duniani kutoka mwaka 2016 hadi 2020.

 

 

/ https://p.dw.com/p/44qVj