Ujerumani ina ushahidi wa uhalifu wa kivita Ukraine
17 Aprili 2023Kwa mujibu wa gazeti hilo la kila Jumapli, ofisi ya polisi yenye kuhusika na uhalifu ya shirikisho la Ujerumani (BKA) imepokea taarifa 337 kuhusu uwezekano wa uhalifu wa kivita nchini Ukraine. Likinukuu takwimu za serikali kuanzia Februari 2022 hadi katikati ya Aprili, gazeti hilo limeandika wachunguzi wamewahoji karibu mashahidi 90 kuhusu ukatili unaodaiwa kufanywa na wanajeshi wa Urusi katika kipindi hiki cha vita vya Ukraine.
Theluthi mbili ya waliohojiwa walikuwa wakimbizi kutoka Ukraine ambao wamekimbilia Ujerumani. Lakini pia vyanzo vingine vilitoka kwa raia wa Ujerumani nchini Ukraine. Kiini cha kutolewa taarifa hiyo na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ujerumani ilikuwa ni ikijibu swali la kibunge kutoka kwa mbunge wa mrengo wa kati kulia Günter Krings.
Taasisi ya ujasusi ya Ujerumani yasaidia uchunguzi Ukraine
Gazeti Welt am Sonntag limesema BKA, taasisi ambayo inalingana na FBI kwa Marekani, imetoa msaada wa kitaalamu kwa wachunguzi wa Ukraine ambao wanajikita katika uhalifu wa kivita. Gazeti hilo lilmeinuku serikali ya Ujerumani ikisema kwamba mamlaka za usalama mjini Kyiv zimepokea nyenzo zitakazoweza kufanikisha upatikanaji wa haraka wa ushahidi na nyaraka.
Kadhalika serikali ya Berlin pia imepeleka vifaa vingine kama magari na rasilimali nyingine za uratibu na uendeshaji vyenye thamani ya jumla ya zaidi ya Euro milioni 11.5, ikiwa sawa na dola milioni 12.8.
Rais Putin anapaswa kushtakiwa
Akijibu ufichuzi huo, Waziri wa Sheria wa Ujerumani Marco Buschmann aliliambia gazeti la Welt am Sonntag kwamba mtu yeyote ambaye, akitolea mfano wa Rais wa Urusi Vladimir Putin, anachochea vita vya umwagaji damu anapaswa kujibu mahakamani inapoaswa ashitakiwe kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.
Waziri huyo aliongeza kwa kusema kwamba hatua hiyo sio tu kwa Putin lakini pia kwa wengine ambao wanahusika na uhalifu mbaya dhidi ya sheria za kimataifa katika ardhi ya Ukraine.
Waendesha mashtaka wa Ukraine wanasema vikosi vya Urusi viliwaua takriban raia 1,400 karibu na Bucha, mji ulio karibu na mji mkuu wa Ukraine, ambapo miili hiyo iligunduliwa mwaka jana baada ya kuondoka kwa wanajeshi wa Urusi.
Soma zaidi: Ukraine waadhimisha mwaka mmoja wa ukombozi Bucha
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya kutetea haki za binadamu na waandishi wa habari, tangu majeshi ya Urusi yalipovamia Ukraine mwezi Februari mwaka jana, yanadaiwa kufanya matendo mabaya sana na madai ya uhalifu wa kivita kwa raia wa taifa hilo.
Chanzo: DW.