1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na mgogoro kuhusu sera ya wakimbizi

13 Juni 2018

Kansela Merkel na waziri wake wa mambo ya ndani Seehofer wako kwenye mvutano mkubwa kuhusu suala la wakimbizi unaotishia kuiporomosha serikali ya muungano

https://p.dw.com/p/2zUrY
Horst Seehofer CSU), Bundesminister für Inneres, Heimat und Bau, und Bundeskanzlerin Angela Merkel (CDU)
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Kansela Angela Merkel anakabiliwa na wakati mgumu kuhusu sera yake ya wakimbizi inayotishia kuiporomosha serikali yake ya mseto. Waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer ambaye yuko kwenye mvutano mkubwa na Kansela Merkel kuhusu suala la wakimbizi amesema yeye na wenzake wa Italia na Austria, Matteo Salvini na Herbert Kicki wameunda ushirikiano wiki hii kukabiliana na wahamiaji haramu, mpango ambao unapingwa na Kansela Angela Merkel.

Mawaziri wa mambo ya ndani wenye msimamo mkali kutoka Austria, Ujerumani na Italia wameunda ushirikiano maalum wa kukabiliana na wahamiaji haramu, hilo ni tangazo alilolitowa leo Kansela wa Austria Sebastian Kurz mjini Berlin, tamko ambalo linauzidisha mvutano uliotanuka barani ulaya kuhusu suala la wahamiaji. Tamko hilo la Kurz limekuja baada ya kukutana na waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer na  linatowa ujumbe mahsusi kwa kansela Angela Merkel ambaye anajaribu kutafuta ushirikiano wa nchi za Umoja wa Ulaya kuhusu mahali pa kuwapeleka wanaotafuta hifadhi.

Deutschland PK Bundeskanzlerin Angela Merkel und österreichischer Bundeskanzler Sebastian  Kurz in Berlin
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Seehofer ambaye yuko kwenye mgogoro wa wazi na Kansela Angela Merkel, mgogoro ambao unatishia hali ya utulivu na masikizano katika serikali ya muungano nchini Ujerumani anasema  ushirikiano wake pamoja na mawaziri wenzake wa ndani wa Italia na Austria utakwenda mbali zaidi na kuyaangalia masuala ya usalama na ugaidi ingawa hakutowa maelezo ya kina kuhusu jinsi lengo hilo litakavyotimizwa.

"Jana nilizungumza na waziri wa mambo ya ndani wa Italia kwa simu na akasema kwamba anatamani kuwepo ushirikiano wa karibu kati ya Rome, Vienna na Berlin, katika ngazi ya mawaziri kukabiliana na masuala kama usalama, ugaidi na uhamiaji, na mimi niliridhia.''

Kansela Angela Merkel ameupinga kwa nguvu zote mpango uliopendekezwa na waziri wake wa mambo ya ndani Seehofer wa kuwarudisha wahamiaji ambao wameshajiandikisha katika nchi nyingine ya Umoja wa Ulaya, wanaofika katika mipaka ya Ujerumani wakitaka kuomba kuingia nchini kuomba hifadhi. Merkel anasema Ujerumani haipaswi kuchukua uamuzi kivyake wakati ambapo Ulaya inatafuta sera ya pamoja kuhusu suala la wahamiaji. Awali alipotembelea klabu ya soka ya SV Rot-Weiss Victoria Mitte mjini Berlin, Merkel alitoa mfano wa jinsi watu wanavyoishi kwa kusema.

"Huu ndio uhalisia. Baadaye  tutakuwa na mkutano wa kilele wa kinadharia kuhusu ujumuishaji wageni katika jamii, ambao utahusu jinsi watu mbali mbali kutoka mataifa tafauti wanavyoishi pamoja, sio kuangazia juu ya wahamiaji lakini watu ambao wanazaliwa hapa Ujerumani. Mfano huu hapa unaonyesha jinsi wasichana kutoka asili mbali mbali wanavyocheza kwa mafanikio pamoja.''

Innenminister Horst Seehofer trifft Sebastian Kurz
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Pamoja na mvutano huo Seehofer leo (13.06.2018) amesisitiza kwa upande wake kwamba amejitolea kutafuta mwafaka juu ya suala hili na Kansela Angela Merkel wiki hii ingawa haijulikani kitu gani kinaweza kutokea. Ama Kansela wa Austria Sebastian Kurz ambaye nchi yake inachukua nafasi ya kupokezana ya mwenyekiti wa Umoja wa Ula Julai mosi amesema anategemea msimamo wake mkali juu ya wahamiaji kuungwa mkono na Uholanzi na Denmark pindi nchi yake inachukua nafasi hiyo ya mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya.

Ikumbukwe kwamba Hungary, Poland, Jamhuri ya Czech na Slovakia zote zimekuwa ama zikikataa moja kwa moja au kupinga kuwapokea wakimbizi chini ya mfumo wa Umoja wa Ulaya wa kugawana wakimbizi unaokabiliwa na upinzani.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW