Ujerumani haitingishwi na machafuko ya dunia - Scholz
31 Desemba 2023Katika ujumbe wake wa Mwaka Mpya, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amekiri juu ya hali ngumu ya kimataifa lakini ameonyesha imani kwamba "Ujerumani itashinda."
"Mateso mengi; umwagaji mwingi wa damu. Ulimwengu wetu umekuwa sehemu isiyotulia na kali zaidi. Inabadilika kwa kasi ya kustaajabisha," Scholz alisema, kulingana na maandishi ya hotuba yake iliyotolewa na ofisi yake kabla ya kutangazwa kwenye mkesha wa mwaka mpya.
"Matokeo yake ni kwamba sisi pia, inabidi tubadilike. Hili ni jambo la kutia wasiwasi kwa wengi wetu. Kwa baadhi, pia linasababisha kutoridhika. Nalitilia maanani hilo."
Kiongozi huyo wa Ujerumani, hata hivyo, alitoa maoni ya matumaini na kuangazia vikwazo ambavyo nchi hiyo ilifanikiwa kushinda mnamo 2023, ndani na kimataifa.
"Nguvu zetu ziko katika utayari wetu wa kuafikiana - katika juhudi tunazoweka kwa ajili ya mtu mwingine," Scholz alisisitiza.
Uchaguzi wa Marekani huenda ukawa na athari kubwa
Huku chaguzi nyingi muhimu zikifanyika duniani kote mwaka wa 2024, hasa Marekani, Uingereza, India na Bunge la Ulaya, Scholz alisisitiza umuhimu wa chaguzi hizi - hasa Marekani - wakati ambapo vita vinaendelea nchini Ukraine na Mashariki ya Kati.
Kansela huyo amesisitiza kuwa nguvu ya Ujerumani iko katika Umoja wa Ulaya. "Ni muhimu sana kwa Ulaya kuibuka ikiwa imeungana na imara kutoka kwenye uchaguzi wa Ulaya katika mwaka ujao," alisema.
Soma pia:Je, ukomo wa deni la Ujerumani ni nini hasa?
"Hata hivyo, vita vya Urusi mashariki mwa bara letu havijakwisha. Wala mzozo wa silaha katika Mashariki ya Kati haujamalizika. Mwaka ujao pia utashuhudia uchaguzi wa rais nchini Marekani, ambao unaweza kuwa na madhara makubwa - ikiwa ni pamoja na kwetu hapa Ulaya."
'Tulidhiti mdororo wa kiuchumi'
Huku mfumuko wa bei ukishuka kutoka wastani wa asilimia 7.9 mwaka 2022 hadi asilimia 3.2 mnamo Novemba 2023, kiwango cha chini kabisa katika miaka miwili, Scholz alizungumza juu ya mtazamo mzuri zaidi wa kiuchumi kuliko mwaka mmoja uliopita - hata wakati kiwango cha mfumuko wa bei cha Ujerumani bado ni cha juu zaidi. kuliko wastani wa asilimia 2.4 katika kanda ya Euro.
Pia alizungumzia usambazaji wa gesi ya Ujerumani iliyojazwa tena, ambayo aliielezea kama "iliyojaa hadi ukingo" na kusema nchi hiyo iliepuka kudorora kwa uchumi.
"Mnakumbuka tulipokuwa mwaka mmoja uliopita?" Scholz aliuliza. "Wataalamu wengi walikuwa wametabiri kushuka kwa uchumi kwa asilimia tatu, nne, tano. Wengi walihofia kuwa bei zingeendelea kupanda. Kulikuwa na wasiwasi kuhusu kukatika kwa umeme na kukosekana kwa joto katikabaadhi ya majumba.
Soma pia:Ujerumani: Waziri wa zamani wa fedha Wolfgang Schäuble afariki dunia
"Mambo yamekuwa tofauti," alihitimisha. "Mfumuko wa bei umepungua. Mishahara na pensheni vinapanda. Mifumo yetu ya kuhifadhi gesi imejaa hadi ukingoni kwa msimu wa baridi."
"Tulizuia mdororo huo wa uchumi," Scholz aliongeza. "Tuliokoa nishati, na tulifanya maandalizi kwa wakati. Sote tulifanya - kwa pamoja."
Matarajio ya mwaka 2024
Scholz, ambaye ni kiongozi wa chama cha Social Democrat cha Ujerumani (SPD), pia alisema serikali ya muungano itaweka kipaumbele katika uboreshaji wa miundombinu ya barabara na reli katika kile alichoeleza kuwa ni hitaji la "kuwekeza kwa nguvu katika siku zijazo."
Chama cha SPD kinatawala kwa pamoja na chama cha Kijani, na kile cha Kiliberali, Free Democrats (FDP).
"Kama mtu yeyote atakuwa amegundua nani anasafiri kwa treni siku hizi, au anakaa kwenye msongamano wa magari kwenye njia ya daraja linalobomoka, nchi yetu imerudishwa nyuma kwa muda mrefu sana," alisema. "Ndio maana tunawekeza sasa - katika barabara nzuri na reli bora."
Soma pia: Scholz: Uamuzi wa EU unapaswa kuwa ishara pia kwa Putin
Lakini alikiri kuwa uamuzi wa Mahakama ya Kikatiba mnamo Novemba kwamba fedha za kukabiliana na athari za janga ambazo hazijatumika hazingeweza kutumika tena kwa miradi ya mazingira na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, "hatutaweza kutekeleza mipango yote tuliyotarajia."
Scholz anaamini kwamba kila mtu nchini Ujerumani ana jukumu muhimu, na kwa kuheshimiana, "hatuhitaji kuwa na hofu juu ya siku zijazo."
"Basi mwaka 2024 utakuwa mwaka mzuri kwa nchi yetu hata kama baadhi ya mambo yatatokea tofauti na vile tunavyowazia leo, usiku wa kuamkia mwaka mpya."