1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani dhidi ya Brazil

4 Agosti 2008

Katika dimba la olimpik jumatano,Ujerumani inaanza dimba na Brazil.

https://p.dw.com/p/EqLT
Marekebu za timu za olimpikPicha: picture-alliance / dpa

Tunamkagua Josiah Thugwane, ambae siku kama leo katika michezo ya olimpik ya Atlanta,1996 aliipatia Afrika kusini, medali yake ya kwanza ya dhahabu ya olimpik kutoka mbio za marathon.

Jumatano hii dimba la olimpik laanza kwa changamoto ya marudio ya finali ya Kombe la dunia la wanawake kati ya mabingwa wa dunia-Ujerumani na makamo-bingwa Brazil.

Stadi wa mabingwa wa Ujerumani-Bayern Munich,mtaliana Luca Toni yamkini asicheze duru ya kwanza ya kombe la Ujerumani mwishoni mwa wiki kwa kuumia goti.

Na timu ya Olimpik ya Tanzania imeondoka leo kwa safari ya Beijing.

►◄

Tuanze na michezo ya Olimpik ya Beijing, itayofunguliwa rasmi ijumaa hii ijayo kwa shangwe na shamra shamra.

Wakati michezo yenyewe itafunguliwa rasmi ijumaa, tayari jumatano hii -siku 2 kabla ya ufunguzi-tutajionea marudio ya finali ya Kombe la dunia la wanwake 2007 kati ya mabingwa-Ujerumani na makamo-bingwa Brazil ikiongozwa na mwanasoka wa mwaka Marta.

Hii ni nafasi kwa Brazil kulipiza kisasi kwa wasichana wa Ujerumani kwa kuwanyima kombe la dunia.

Marekani, mabingwa wa Olimpik wa medali ya dhahabu katika michezo ya 2004 mjini Athens,Ugiriki pia wana mtihani mgumu siku hiyo wakianza na Norway.

Ujerumani iliizaba Brazil mabao 2:0 katika finali ya mwaka jana ya kombe la dunia lililochezwa pia nchini China pale Marta, mchawi wa dimba wakike wa Brazil, alipokosa kutia bao la penalty na Brazil kuipoteza nafasi nyingi za kutia mabao.

Brazil walishindwa pia katika finali ya olimpik ya 2004 na marta mara hii anaamini watapiga hatua moja zaidi.

Brazil na ujerumani zimeangukia kundi moja F linalojumuisha Nigeria na Korea ya Kusini .Nigeria, ni mabingwa wa olimpik wa dimba 1996 huko Atlanta.

Mabingwa wa olimpik-marekani wanashirki katika dimba la olimpik bila ya mshambulizi wao Abby Wambach,alievunjika mguu wakati wa mechi ya kirafiki na Brazil mwezi uliopita.

Wambach amepachika mabao 99 katika mechi 127 kwa marekani pamoja na lile balo la ushindi dhidi ya Brazil katika finali ya olimpik mjini Athens, 2004.

Wenyeji wasichana wa China wana miadi na Sweden huko Tianjin.

RIADHA NA OLIMPIK:

Miaka 12 iliopita siku kama leo, mwanariadha wa Afrika kusini, Josiah Thugwane, aliandika historia ya olimpik kwa nchi yake alipotimka mbio katika marathon na kuipatia Afrika kusini, medali yake ya kwanza ya dhahabu kunyakuliwa na muafrika kusini mweusi.Muda wake wa ushindi ulikua masaa 2:12.36 akija sek .3 tu mbele ya mkorea wa Kusini Lee Bong ju.

Thugwane alisema baada ya ushindi wake kwamba kushinda yeye kumeonesha kwamba waafrika nchini Afrika Kusini sasa wamekuwa huru baada ya kukata pingu za "siasa ya ubaguzi na mtengano ".

Mwishoni mwa wiki, tokeo jengine la historia ya karibuni ya olimpik ni

kupokonywa timu ya Marekani ya mbio za mita 4X400 medali zao za dhahabu walizonyakua katika mbio hizo huko Sydney, Australia mwaka 2000.

Hii inatokana na madhambi ya doping-matumizi ya madawa ya mmoja kati ya wanariadha hao 4-Antonio Pettigrew.

Halmashauri kuu tendaji ya Kamati ya olimpik ulimwenguni ilipitisha hukumu hiyo ya kuivua taji timu hiyo kabla kuanza ijumaa hii kwa michezo ya 29 ya olimpik ya Beijing.Timu hiyo ya Marekani mbali na Pettigrew,iliingiza mabingwa Michael Johnson na ndugu wawili-Alvin na Calvin Harrison.

Pettigrew aliungama karibuni kwamba, alitumia madawa kuanzia 1997.

Timu ya Olimpik ya wanariadha 10 ya Tanzania,iliondoka leo Dar-es-salaam kwa safari ya Beijning ikitumai kurejea na medali za kwanza za olimpik tangu Philbert Bayi,bingwa wa zamani wa rekodi ya dunia ya mita 1500 na Suleiman Nyambui, kunyakua medali za fedha za Olimpik katika michezo ya Moscow, 1980.Kati ya wanariadha hao 10 wawili wanashiriki katika mashindano ya kuogolea.

DIMBA:Kinyan'ganyiro cha kuania kombe la klabu bingwa barani Afrika kiliendelea mwishoni mwa wiki:

Mabingwa wa zamani Enyimba ya Nigeria na Zamalek ya Misri wote wawili walitamba nyumbani hapo jana.

Mtiaji mabao mengi katika kombe hili Stephen Worgu alikua miongoni mwa wale waliotikisa wavu pale Enyimba ilipoikomea Conton Sport ya Kamerun mabao 2:0 mjini Aba.

Mabingwa mara 5 Zamalek walitia bao na mapema ili kuzima vishindo vya Dynamo ya Zimbabwe na kuwatoa kwa bao 1:0 nyumbani Cairo.

Siku moja kabla- jumamosi, mabingwa wengine mara 5 kama Zamnalek-Al Ahly, pia ya Misri walitoka sare 0:0 na ASEC Abidjan ya Ivory Coast. Al Hilal ya Sudan pia ilimudu suluhu ya 0:0 na TP Mazembe ya jamhuri ya kidemokrasi ya kongo.

duru ijayo ya kombe la klabu bingwa itakua August 15.

Tottenham Hotspurs iliizaba Borussia Dortmund mabao 3-0 hapo jana na kutwaa kombe la kuadhimisha miaka 50 tangu kuasisiwa kwa Feynoord Rotterdam.Tottenham ilioichapa Celtic hapo ijumaa 2-0 ilimaliza nafasi ya kwanza kileleni kwa pointi 6.Celtic ikamaliza wapili.

Stadi wa Bayern Munich na mshambulizi wa timu ya Taifa ya mabingwa wa dunia-Itali, Luca Toni, ameumia na yaonesha Bayern Munich itabidi kucheza jumamosi ijayo katika duru ya kwanza ya kombe la taifa la Ujerumani bila ya Luca Toni.

Luca Toni hakuwa uwanjani pale Bayern Munich ilipoikomea Urawa Red Diamonds ya Japan mabao 4:1 alhamisi iliopita.

Real Madrid ya Spain nayo imeongeza kitita chake kwa klabu ya Hamburg ili imuachie stadi wake kutoka Holland, Rafael van der Vaart kujiunga na Real Madrid.Hamburg iliarifu hapo jumamosi kwamba fedha ilizopendekeza Real hazitoshi.