Ujerumani bado ipo kwenye mkwamo wa kisiasa
1 Desemba 2017Rais Frank Walter Steinmeier nchini Ujerumani alikutana na viongozi wa kundi la wahafidhina la vyama vya Christian Democratic Union, CDU na Christian Social Union, CSU, linaloongozwa na Kansela Merkel na chama cha Social Democratic SPD. Mkutano huo ulilenga kujaribu kutafuta njia za kuumaliza mkwamo wa kisiasa na hatimae kuunda serikali ya pamoja.Hata hivyo mazungumzo hayo yanaelekea hayakuzaa matunda.
Waziri wa mambo ya nje akitokea chama cha SPD Sigmar Gabriel alisema wazi kwamba chama chake hakitoridhia kirahisi kuingia katika serikali nyingine ya muungano na kundi la Kansela Angela Merkel.Akizuungumza na shirika la habari la Ujerumani ZDF Gabriel alisema watu hawapaswi kukitarajia chama chake ambacho kwahakika bado kimo ndani ya serikali inayoondoka ,kukubali haraka kujiunga kwa mara nyingine na serikali ya muungano na vyama vya CDU na CSU kutokana na kushindwa kufikiwa makubaliano ya kuunda kile kilichoitwa serikali ya Jamaica.
Waziri huyo wa mambo ya nje pia anasema kwamba kwa hivi sasa ni juu ya wahafidhina kuonesha kile haswa wanachokitaka huku akiongeza kusema kwamba kundi hilo la Kanselsa Merkel limekaa chini kwa kipindi cha miezi kadhaa pamoja na wanamazingira au chama cha kijani na waliberali chama kinachopendelea biashara cha FDP bila ya kufanikiwa kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya pande tatu,na kwahivyo sasa ni wajibu wa kila mmoja kutowatia kishindo SPD kukubali kuingia katika makubaliano ya kuunda serikali.
Kansela Merkel anajaribu kutafuta mshirika wa kuunda nae serikali tangu ulipomalizika uchaguzi mkuu Septemba 24 ambako kundi lake la siasa za wastani za mrengo wa kulia kuonekana kuunga mkono mrengo wa siasa kali katika uchaguzi huo.Chama cha SPD ambacho kwa upande wake kimekuwemo ndani ya serikali ya Kansela Merkel kuanzia mwaka 2013 hadi sasa kilipata pigo kubwa katika matokeo ya uchaguzi huo,pigo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya chama hicho tangu baada ya vita vya pili vya dunia,kimepinga tangu mwanzo kujiunga tena na serikali ya muungano na Merkel.
Lakini baada ya kiongozi wa chama hicho Martin Schulz kushinikizwa na rais Frank Walter Steinmeier ambaye pia aliwahi kuwa waziri wa mambo ya nje akiwa chama hicho cha SPD kubadili msimamo,alionekana kuwa tayari kujadiliana juu ya mwelekeo wa kuumaliza mkwamo huo wa kiasiasa.Hata hivyo baada ya hapo jana kukaa kwa masaa mawili kwenye mkutano na kundi la Merkel hakuna hatua yoyote kubwa iliyopigwa.Ingawa leo Ijumaa vyama vyote hivyo SPD ,CDU na CSU vitakutana katika mkutano wa viongozi wa ngazi ya juu kujadiliana vipi kuendelea mbele ama wakubaliane kuunda serikali au kuitisha uchaguzi mwingine.Inatajwa lakini kwamba chama cha SPD hakitarajiwi kuridhia kuanza mazungumzo rasmi ya kuunda serikali hadi pale kitakapofanya mkutano wake mkuu wiki ijayo.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: Josephat Charo