Ujenzi wa Mali bila ya amani?
15 Mei 2013Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Laurent Fabius, anasema lengo ni kuijenga upya Mali kwa sababu mambo sasa yanaenda vizuri. Ameyasema hayo mbele ya wajumbe kutoka nchi 100 wanaohudhuria mkutano huo mjini Brussels.
Ujerumani pia inawakilishwa kwenye mkutano huo. Kansela Angela Merkel alisisitiza umuhimu wa mkutano huo juu ya kuijenga upya Mali pale alipokunata na Rais wa Niger wiki iliyopita.
Wakati huo huo mgogoro baina ya serikali kuu mjini Bamako, kusini magharibi mwa Mali na waasi wa Kitaureg wa kaskazini mashariki bado unaendelea. Kwa mujibu wa taarifa, wanajeshi wa serikali wameelekea katika mji wa Kidal na wameshaondoka mji wa Gao na wakielekea kaskazini mashariki.
Hata hivyo, Luteni Kanali Diaran Kone wa jeshi la serikali hakutaka kutoa taarifa yoyote katika mahojiano yake na DW. Kwa sasa mji wa Kidal bado umo katika mikono ya waasi wa MNLA, chama cha ukombozi cha kabila la Kitaureg.
Kidal kukombolewa?
Mjumbe wa jamii za watu wanaotishiwa kutoweka Ulrich Delius ameeleza matumaini kwamba mji wa Kidal utakombolewa wakati mkutanowa mjini Brussels ukiendelea. "Mtu anapaswa kuangalia kwa makini jinsi majeshi ya serikali yanavyokabiliana na wapiganaji wa Kitaureg, wenye silaha na wale wasiokuwa na silaha.Tunahofia kutoa mashambulio zaidi."
Katika harakati za kuikomboa miji na vijiji katika eneo la Wataureg raia mia nnne wameshauwa hadi sasa. Mji wa Kidal unazingatiwa kuwa ngome kuu ya waasi wa MNLA wanaopigania kuwa na sehemu yao na kujitawala.
Fabius amesema kwa jumla usalama unaimarika nchini Mali na kwamba kinachohitajika sasa ni demokrasia, mdahalo na maendeleo yote kwa pamoja. Lakini amesema ili kuyafikia malengo hayo fedha zitahitajika.
Ufaransa ilipeleka majeshi yake nchini Mali mnamo mwezi wa januari ili kupambana na waislamu wenye itikadi kali wenye uhusiano na mtandao wa Al-Qaeda walioiteka sehemu ya kaskazini. Waasi waliitumia fursa iliyotokana na kuangushwa kwa serikali.
Uchaguzi nchini Mali
Mali inatarajia kuitisha uchaguzi mnamo mwezi wa Julai ili kuchagua serikali kwa matumaini kwamba serikali hiyo itaiondoa Mali kutoka kwenye mgogoro.
Waasi waliyashinda majeshi ya serikali na kusababisha kuangushwa kwa serikali.Waasi wa kitauregi waliutumia mwanya huo kuiteka sehemu ya kaskazini.Waasia hao walishirkiana na washira wao-waislamu wenye itikadi kali.
Hata hivyo waislamu hao baadae waliwageuka waasi wa kitauregi.
Lakini majeshi ya Ufaransa yaliingilia kati na kuwatimua waasi kwenye miji muhimu:
Waasi hao wamekimbilia jangwani na katika maficho kadhaa.Na sasa wanapigana vita vya kuvizia na kushambulia.Hata hivyo Waziri wa mambo ya nje wa a Ufaransa bwana Fabius amesema mapigano nchini Mali yanakaribia kumalizika.
Ameeleza kwamba majeshi ya Ufaransa yanakaribia kushinda vita na kilichobakia ni kuleta amani kwa njia ya maendeleo ya uchumi.
Mkutano wa mjini Brussels juu ya kuijenga upya Mali unahudhuriwa na wakuu wa nchi kadhaa.
Marais wa Ufaransa na Mali ndiyo watakaokuwa wenyeviti wa pamoja wa mkutano.
Mwandishi: Peter Hille
Tafsiri: Mtullya Abdu
Mhariri: Abdul-Rahman, Mohamed