Uingereza yatetea uamuzi wa kuwalipa wafungwa wa Guantanamo
17 Novemba 2010Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Uingereza, William Hague, ameutetea uamuzi wa kuwalipa fidia ya thamani ya mamilioni ya paundi, wafungwa wa zamani wa jela ya Guantanamo. Akiyatembelea makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani, waziri Hague amekiri kuwa kama kesi za wafungwa hao zilizokuwa mahakamani zingeendelea, zingefichua taarifa ambazo zingehataraisha mashirika ya ujasusi. Wafungwa hao wa zamani wa Guantanamo, ambao ni raia au wakaazi wa Uingereza, inadaiwa waliteswa wakati wa vita dhidi ya ugaidi vilivyoongozwa na Marekani, huku mashirika ya usalama ya Uingereza yakifahamu na hata wakati mwingine kushiriki kwenye mateso hayo.
Waziri wa sheria wa Uingereza, Kenneth Clarke anasema makubaliano hayo yaliyofikiwa nje ya mahakama yatayalinda mashirika ya usalama yanayohusika. Clarke aidha amesema makubaliano hayo yanafungua mlango kwa uchunguzi kubaini ikiwa mashirika ya usalama ya Uingereza yalijua kuhusu kuteswa kwa washukiwa katika nchi za kigeni.