Uingereza yataka kubadilishana makombora na Ujerumani
25 Januari 2024Gazeti la Handelsblatt limenukuu vyanzo vya serikali na kidiplomasia vikisema kuwa wiki kadhaa zilizopita, serikali ya Uingereza ilikuwa imependekeza kwa Ujerumani kwamba inaweza kusafirisha makombora aina ya Storm Shadow kwa Ukraine, na kwa upande wake, kupokea makombora aina ya Taurus ya Ujerumani.
Ofisi ya kansela wa Ujerumani yafanyia tathmini pendekezo
Ripoti hiyo imeongeza kuwa ofisi ya Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz imekuwa ikifanyia tathmini pendekezo hilo.
Chanzo cha karibu na mazungumzo hayo, kimesema kuwa ubadilishanaji huo wa makombora unaopendekezwa huenda ukapata uungwaji mkono nchini Ujerumani.
Soma pia:Ukraine yasema ina uhakika Ujerumani itaipatia makombora ya Taurus
Hata hivyo serikali ya Ujerumani imekataa kutoa tamko lolote kuhusiana na ripoti hiyo.
Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Uingereza, amesema kuwa nchi hiyo na washirika wake ikiwa ni pamoja na
Ujerumani zinaendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kuipa Ukraine silaha bora kuiwezesha kutetea eneo lake.