1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchakato kumpata Waziri Mkuu mpya watakiwa kuanza haraka

29 Juni 2016

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaokutana katika mkutano wa kilele mjini Brussels, Ubeligiji, wamekubaliana kuwa Uingereza inahitaji muda kujipanga kabla ya kuanza mchakato wa kujitoa rasmi katika Umoja huo.

https://p.dw.com/p/1JFP0
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaokutana katika makao makuu ya Umoja huo mjini Brussels.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaokutana katika makao makuu ya Umoja huo mjini Brussels.Picha: picture alliance/abaca

Katika mkutano huo, ambao pia ulihudhuriwa na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, aliepata nafasi ya kukutana ana kwa ana na viongozi wa Umoja wa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu kufanyika kwa kura ya maoni wiki iliyopita, viongozi wa umoja huo walitoa mwito kwa Uingereza kutopitisha muda mrefu kabla ya kuanza mchakato huo wa kujitoa. Baada ya majadiliano yaliyochukua saa kadhaa, Rais wa Umoja wa Ulaya, Donald Tusk, alisema anaelewa fika kuwa Uingereza inahitaji muda ili kusubiri hali iweze kutulia nchini humo kutokana na kishindo kilichotokana na matokeo ya kura hiyo ya maoni ndipo iweze kuendelea na hatua inayofuta.

Katika matokeo hayo ya kura ya maoni iliyopigwa Alhamisi ya wiki iliyopita kundi linalounga mkono Uingereza kuondoka kwenye Umoja wa Ulaya lilishinda kwa kupata asilimia 52 ya kura, huku wale wanaotaka kubakia wakipata asilimia 48 , tayari yameibua hisia tofauti nchini humo, ambapo baadhi ya wafuasi wa kundi linalotaka kubakia waliingia katika mitaa ya mji wa London kupinga matokeo ya kura hiyo huku pia wakipeperusha bendera na mabango yaliyosomeka 'Stop Brexit' wakiwa na maana ya kusimamisha hatua hiyo ya kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya.

Cameron atakiwa kuharakisha mchakato wa kumpata Waziri Mkuu mpya

Aidha Umoja wa Ulaya umemtaka Waziri Mkuu David Cameron, ambaye wiki iliyopita alitangaza kujiuzulu wadhifa huo kuharakisha mchakato wa kumpata Waziri Mkuu mpya na hatimaye kuwezesha mchakato huo wa kujitoa upate kuanza.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron
Waziri Mkuu wa Uingereza, David CameronPicha: Reuters/P. Rossignol

Wanasiasa ambao tayari wameanza kutajwa kushika wadhifa huo wa Waziri Mkuu ni pamoja na meya wa zamani wa London, Boris Johnson, ambaye aliongoza kampeni ya kujitoa kwenye umoja huo na Waziri wa Mambo ya Ndani Theresa May.

Kwa upande wake, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, John Kerry, alisema hapo jana kuwa uamuzi uliotokana na matokeo ya kura ya maoni ya kujitoa kwa Uingereza katika Umoja huo wa Ulaya unaweza usitekelezeke na kuwa Uingereza haina haja ya kuwa na haraka ya kuondoka kwenye Umoja wa Ulaya.

Akizungumza ikiwa ni siku moja baada ya kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron , Waziri Kerry alisema Waziri Mkuu David Cameron anajihisi kama mtu asiye na nguvu kuzungumzia jambo ambalo asingelipenda litokee. Marekani ambayo kwa muda mrefu ni mshirika wa karibu wa Uingereza ilionekana kushangazwa na hatua hiyo ya Uingereza kupiga kura ya kuamua kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya.

Wakati huohuo chanzo kimoja cha habari ambacho hakikutaka kuwekwa wazi, kimemkariri Cameron akitaka Umoja wa Ulaya kufikiria kufanya mageuzi katika sheria zinazohusiana na uhuru wa kusafiri ili kuimarisha mahusiano na Uingereza katika siku zinazo kuja pindi hatua hiyo ya kujitoa itakapokuwa imetekelezwa.

Cameron ambaye alirejea Uingereza hapo jana amesema Uingereza na mataifa ya Umoja wa Ulaya yanapaswa kuendelea kuwa na mahusiano ya karibu katika nyanja za kiuchumi na kuwa ili hilo liweze kufikiwa, basi suala la uhuru wakusafiri ni lazima lizingatiwe.

Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE

Mhariri: Bruce Amani