Uingereza yapendekeza kufutwa rekodi za riadha
11 Januari 2016Shirikisho la riadha duniani - IAAF, lilitangazaa mapendekezo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kupigwa marufuku kwa muda mrefu wanariadha watakaopatikana na hatia na pia kuwepo kwa sajili rasmi ya wanariadha waliopatikana na hatia ya kosa hilo.
Mwenyekiti wa UKA, Ed Warner amesema huu ni wakati wa kufanya mabadiliko makuu, akisema kuwa hadhi na heshima ya mchezo huo iliharibiwa kwa kiasi kikubwa katika mwaka wa 2015.
Katika miezi ya hivi karibuni, riadha duniani imekumbwa na dosari hasa kufuatia taarifa kadhaa kuhusu utumizi wa madawa ya kusisimua misuli.
Rais mpya wa IAAF, Sebastian Coe ameapa kuimarisha juhudi za kupambana na matumizi wa dawa zilizopigwa marufuku michezoni, na pia amedokeza kuwa atabuni kitengo maalum kupambana na tatizo hilo kabla ya michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa mjini Rio mwaka huu.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohamed Khelef