Uingereza yamfurusha mwanadiplomasia wa Israel
24 Machi 2010Uingereza imemfukuza afisa katika ubalozi wa Israel nchini humo kutokana na kile kilichotajwa kama matumizi mabaya ya pasi za usafiri za Uingereza yasiyoweza kuvumiliwa, katika mauaji ya kamanda wa kundi la Hamas mjini Dubai. Haya yanajiri wakati kuna hali ya wasiwasi kuhusu kashfa ya mauaji hayo.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Milliband alisema kulikuwa na sababu za kutosha kudhihirisha kwamba Israel ilihusika katika kughushi pasi za usafiri zilizotumiwa na kundi lililomuua kamanda wa Hamas, Mahmud al-Mabhuh mjini Dubai mwezi Januari. Milliband akizungumza bungeni, alisema kwamba tukio linakera sana.
Waziri wa mambo ya nje wa Israel, Avigdor Lieberman alisema alisikitishwa sana na kuondolewa huko kwa afisa wa Israel katika ubalozi wake nchini Uingereza lakini afisa serikalini amesema Israel haiwezi kulipiza kisasi.
Bw.Milliband hakusema ni afisa wa ngazi gani aliyefurushwa lakini taarifa katika magazeti ya Times na Telegraph za Uingereza zinasema kwamba ni afisa wa ngazi ya juu katika idara ya ujasusi ya Israel, Mossad.
Mossad imelaumiwa pakubwa kwa kuhusika katika mauaji ya kamanda wa Hamas lakini Israel inasisitiza kwamba hakuna ushahidi kudhibitisha madai hayo.
Hamas imefurahia kufukuzwa huko kwa afisa huyo kutoka Uingereza na imesema kwamba inatarajia viongozi wa Israel watafunguliwa mashtaka kutokana na kesi mauaji hayo. Washukiwa wa mauaji walitumia pasi walizoghushi kumi na mbili za raia wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Ireland.
Gazeti la Yedioth Ahronoth lenye umaarufu mkubwa nchini Israel na kituo cha redio cha kijeshi nchini humo, zimenukuliwa zikisema kwamba nafasi ya afisa huyo aliyefurushwa itachukuliwa na afisa mwingine na kwamba uhusiano baina ya Israel na Uingereza haujaharibika kabisa.
Waziri wa mambo ya nje wa Australia Stephen Smith amesema anatarajia kupewa ripoti ya kashfa hiyo na Uingereza kwa uchunguzi zaidi.Pasi za Australia pia zilitumiwa na washukiwa wa mauaji hayo.
Mwandishi, Peter Moss/Reuters/AP
Mhariri, Abdul-Rahman Mohammed