1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza yakumbuka mauwaji ya 2005

7 Julai 2015

Leo imetimia miaka kumi tangu kufanyika kwa shambulizi la kigaidi la kujitoa muhanga mjini London Uingereza la mwaka 2005, lililouwa watu 52 na kujeruhi takriban 700.

https://p.dw.com/p/1Ftus
Großbritannien Gedenken an die Terroranschläge von 2005 in London
Picha: Reuters/P. Nicholls

Kuikumbuka siku hiyo David Cameron ameongoza ibada ya kuwakumbuka marehemu hao katika bustani ya Hyde Park mjini London.

Waziri mkuu David Cameron amesema, kuwa leo nchi yake inawakumbuka wahanga wa moja ya shambulizi mbaya kabisa la kigaidi lililowahi kufanyika nchini humo.

Kumbukumbu hiyo inafanyika wiki mbili baada ya shambulizi la kigaidi nchini Tunisia liliouwa watu 38, na 30 kati yao wakiwa waingereza.

"Imeshatimia miaka 10 tangu mauaji ya tarehe saba Julai mjini London na kitisho cha ugaidi kinaendelea kuwepo. Mauwaji ya watalii wa kiingereza 30 nchini Tunisia ni ukumbusho wa ukatili wa vitendo hivyo. Lakini hatutatishwa na ugaidi," Cameron alisema hayo wakati anahutubia katika kumbukumbu hiyo.

Kulikuwa na maombolezi ya dakika moja ya ukimya mjini London leo mchana, ukiwa ni wakati wa kutafakari. Ibada nyengine kadhaa za kumbukumbu zimefanyika kwengineko, ikiwemo ambayo mwanamfalme Charles anapanga kuhudhuria baadae leo. Mabomu matatu yalifyatuliwa wakati mmoja na la nne likaripuka baadae kwenye basi. Shambulio la tarehe saba Julai 2005, lilifanywa na vijana wane kutoka Luton, mji ulioko kilomita 80 kutoka London ambao waliwasili kwenye kituo cha treni wakiwa na mikoba mgongoni iliojaa miripuko.

Maafisa wa kupambana na ugaidi walisema vijana hao wanne walikuwa wafuasi wa itikadi kali ya kiislamu wa nadharia iliokuwa na mafungamano na makundi yenye mafungamano na mtandao wa Al Qaeda nchini Pakistan na Afghanistan. Vijana wote wane walikufa wakati wa shambulizi lao.

Mwandishi: Yusra Buwayhid, dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman