Uingereza yaitaka Iran kuiachia meli yake ya mafuta
22 Julai 2019Waziri wa mambo ya kigeni Jeremy Hunt anapanga kulifahamisha bunge siku ya Ijumaa kukamatwa kwa meli ya mafuta ya Stena Impero pamoja na wafanyakzi wake 23, ambao hivi sasa wako katika bandari ya Iran yenye ulinzi mkali.
Pia leo Jumatatu, Iran ilitoa vidio mpya inayoonesha wafanyakazi wa meli hiyo kwa mara ya kwanza, ikiwa ni jaribio la kuonesha kwamba hawajadhurika.
Hakuna hata raia mmoja wa Uingereza, lakini wengi wao ni kutoka India na pia Ufilipino, Urusi na raia wa Latvia.
Msemaji rasmi wa May , James Slack , amesema Iran imeikamata meli hiyo kwa kutumia visingizio vya uongo na ni kinyume na sheria na inahitaji kuiachia pamoja na wafanyakazi wake mara moja.
Amesema hakuna mpango wa kuzipatia meli zote zinazotembea zikipeperusha bendera ya Uingereza msaada wa kuzisindikiza, kwasababu ya wingi wa meli hizo. Lakini amekana kuwa kubana matumizi kumesababisha jeshi la majini kuwa dogo mno.
Uingereza inatafakari njia mbali mbali za kuongeza mbinyo wa kidiplomasia na kiuchumi kwa Iran, lakini maafisa wanasema operesheni za kijeshi halifikiriwi kwa wakati huu. Uingereza pia inatafuta kuungwa mkono kutoka kwa washirika muhimu wa Ulaya katika juhudi za kuliweka eneo la mlango bahari wa Hozmuz wazi kwa ajili ya meli.
Uchochezi wa mzozo
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas amesema ana wasiliana kwa karibu na mataifa ya Umoja wa Ulaya kama Ufaransa na Uingereza katika mzozo na Iran. Amesema mataifa ya magharibi hayapaswi kuuchochea zaidi mzozo huu.
"Kwetu sisi ni muhimu kwamba, pamoja na hatua za kuzuwia hatari katika mlango bahari wa Hormuz, kadi ya kidiplomasia ni lazima iendelee kutumika. hususan, naamini kwamba ni muhimu kuzileta nchi za ghuba katika meza moja katika wakati fulani kujadili masuala ya usalama baharini. Kila kitu ni lazima kiwekwe akilini na tusichukua hatua ambazo zitachangia katika kuuchochea mzozo huu. Kile tunachohitaji ni kutouchochea mzozo. Na hili pia ni wazo la wenzetu wa Uingereza na Ufaransa."
Wakati huo huo mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Oman atakwenda Iran mwishoni mwa juma hili, mnamo wakati ambapo Oman imekuwa na uhusiano mzuri na Iran katika wakati wote wa mizozo mbali mbali ya kikanda, na kuruhusu wakati fulani kuwa mpatanishi, ikiwa ni pamoja na hata katika mizozo inayoihusu Marekani na mataifa ya ghuba.
Rais wa Marekani nae amekana madai ya Iran kuwa imevunja genge ya makachero wa CIA na kuwakamata watuhumiwa 17 waliodaiwa kuwa wana mahusiano na shirika la ujasusi la Marekani CIA.