Uingereza yaapa kumkamata Assange
17 Agosti 2012Bado Julian Assange ameendelea kujificha ndani ya ubalozi wa Ecuador jiini London, ambapo polisi nao wanaendelea kulinda lango la kutokea ubalozi huo.
Shirika la habari la AFP linaripoti kuwashuhudia kiasi ya polisi 10 waliowekwa nje ya ubalozi huo mapema leo, tayari kumkamata Assange, ambaye amejipatia umaarufu kwa kuziweka hadharani nyaraka za siri za balozi za Marekani kupitia mtandao wake wa WikiLeaks, kitendo ambacho Marekani inadai kinahatarisha usalama wake.
Mtandao wa WikiLeaks umelaani kuendelea kuwapo kwa polisi nje ya ubalozi huo, ukikuita kuwa ni "mbinu za vitisho." Wafuasi wa Assange walipiga kambi ubalozini hapo kwa usiku mzima, wakiwa wamelala kwenye vipande vya maboksi.
Uingereza imeshaonya tangu jana kwamba mgogoro huu wa kidiplomasia huenda ukachukua miaka mingi kumalizika, huku nayo Ecuador ikishikilia kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa zinazochunga mahusiano ya kibalozi.
Rais Rafael Correa wa Ecuador, anayemchukulia Assange kama alama ya uhuru wa maoni unaopiganiwa na mataifa ya magharibi, amesema Uingereza ina wajibu wa kuheshimu mamlaka na uhuru wa Ecuador.
Akiandika kwenye mtandao wa Twitter muda mchache kabla ya uamuzi wa nchi yake kutangazwa hapo jana, Rais Correa alisema "hakuna yeyote ambaye ataitisha Ecuador."
Uingereza yaapa kumkamata Assange
Lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, William Hague, amesema nchi yake itatekeleza wajibu wake wa kisheria kwa kumkamata Assange.
"Chini ya sheria zetu, baada ya Bwana Assange kumaliza mbinu zote za kukata rufaa, mamlaka za Uingereza zina wajibu wa kumpeleka Sweden. Nasi lazima tutekeleze wajibu huo, na bila ya shaka tumedhamiria kikamilifu kufanya hivyo."
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na WikiLeaks kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, Assange atatoa taarifa yake nje ya ubalozi huo hapo Jumapili, ingawa haikusemwa ikiwa ataondoka kwenye jengo la ubalozi au la.
Uingereza kuvunja sheria za kimataifa?
Katika taratibu za kawaida za kidiplomasia, majengo ya balozi yanachukuliwa kama eneo la nchi yenye ubalozi husika na mtu hawezi kuingia bila ya ruhusa ya nchi hiyo. Lakini hapo jana Uingereza iliikasirisha Ecuador ilipoonesha kwamba ingelitumia sheria zake za ndani kuvunja sheria za kimataifa na kuingia ndani kumkamata Assange.
Hata hivyo, mwakilishi wa Uingereza nchini Ecuador, Philip Barton, amesema Uingereza inataka kupatikana suluhisho la mgogoro huu kwa njia ya makubaliano.
Jumuiya ya Mataifa ya Amerika imesema itaamua hivi leo ikiwa iitishe mkutano wa mawaziri wake wa nje kuhusiana na sakata hili. Uingereza ina hadhi ya mjumbe mwangalizi kwenye Jumuiya hiyo.
Tayari Ecuador imeshaitisha mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Mataifa ya Amerika ya Kusini unaotarajiwa kufanyika Jumapili.
Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Ricardo Patino, alisema nchi yake ilifikia uamuzi wa kumpa hifadhi Assange, baada ya Uingereza, Sweden na Marekani kukataa kutoa uthibitisho mwanzilishi huyo wa mtandao wa WikiLeaks hatokabidhiwa kwa Wamarekani baada ya kuingia mikononi mwa Sweden.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Othman Miraji