1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza yaanza mashambulizi Syria

3 Desemba 2015

Uingereza imefanya mashambulizi ya kwanza ya kutokea angani nchini Syria mapema leo (03.12.2015) na hivyo kujiunga na muungano unaongozwa na Marekani unaopambana na kundi la Dola la Kiislamu IS nchini Syria.

https://p.dw.com/p/1HGBv
Zypern Britische Luftwaffe greift Stellungen des IS in Syrien an
Picha: Getty Images/M. Cardy

Ndege nne za jeshi la anga la Uingereza Royal Air Force, zimeondoka kambi ya jeshi ya Akrotiri nchini Cyprus muda mfupi baada ya wabunge 397 kupiga kura kuyaunga mkono mashambulizi dhidi ya wanamgambo wa kundi hilo, huku wabunge 223 wakipinga.

Msemaji wa wizara ya ulinzi alisema ndege hizo zimefanya mashambulizi ya kutokea angani Syria na kurejea kambini. Waziri wa ulinzi wa Uingereza Michael Fallon amesema ndege za Tornado zilifaulu kuyashambulia maeneo ya mafuta katika viwanja vya Omar.

Jeshi la anga la Uingereza limekuwa likifanya mashambulizi ya kutokea angani dhidi ya IS nchini Iraq tangu mwaka 2014. Uamuzi wa kuitanua operesheni hiyo hadi Syria umekuja baada ya mjadala wa muda wa masaa kumi na nusu bungeni ambapo waziri mkuu David Cameron alijenga hoja akisema lazima Uingereza iwashambulie wanamgambo wa kundi hilo katika ngome zao badala ya kukaa kitako kusibiri wawashambulie Waingereza.

Cameron aliyapongeza matokeo ya kura bungeni akiandika katika mtandao wa Twitter: "Naamini bunge limepitisha uamuzi sahihi kuilinda Uingereza - harakati ya kijeshi Syria kama sehemu ya mkakati mpana."

Rais wa Marekani Barack Obama pia aliupongeza uamuzi huo akiieleza Uingereza kuwa mojawapo ya washirika muhimu katika mapambano dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu.

Großbritannien Rede Cameron zur IS Bekämpfung im Parlament
Bunge la Uingereza katika kikao chakePicha: picture alliance/empics

Akizungumza muda mfupi baada ya bunge kuridhia mashambulizi nchini Syria waziri wa mambo ya nje wa Uingereza, Philipp Hammond, alisema wanayatumia mashambulizi hayo kulidhibiti na kulivunja nguvu kundi la Dola la Kiislamu mjini Raqqa na watafuatilia mchakato wa kisiasa kujaribu kuutanzua mzozo wa Syria.

Hammond pia alisema, "Wakati wa harakati ya ardhini Raqqa utawadia pale serikali ya mpito itakapokuwepo Syria kwa sababu watu wote tunaowahitaji kupambana na wanamgambo wa Dola la Kiislamu wanapigana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Tunahitaji washirikiane bega kwa bega kuikomboa nchi yao inayokaliwa na wanamgambo hawa."

Upinzani wakosa msimamo wa pamoja

Chama kikuu cha upinzani cha Labour kiligawika kuhusu suala hilo. Mwenyekiti wa chama hicho, Jeremy Corbyn, anayewakilisha kundi la mrengo wa shoto la chama hicho, alizungumzia kile alichokiita "uingiliaji kati haraka kijeshi na usiojali."

Lakini wabunge zaidi ya 60 wa chama hicho, wakiwemo maafisa wa vyeo vya juu, walipiga kura kuyaunga mkono mashambulizi nchini Syria, hatua ambayo inazidisha mpasuko ndani ya chama cha Labour.

Fauka ya hayo mbunge wa chama cha Labour na waziri kivuli wa maendeleo ya kimataifa, Diane Abbott, alisema, "Kwanza ningesema chama kwa ujumla hakijagawika. Lakini pia niseme wazi kwamba upigaji kura huu umekuwa wa kusikitisha. Tunaotakiwa kuwafikiria ni watu wa Raqqa wakati ndege hizo zitakaporuka katika angao yao katika saa 24 zijazo."

Maafisa wa Uingereza walisema ndege za kivita za jeshi la anga aina ya Typhoon na Tornado, zikiwa na makombora aina ya Brimstone yanayoweza kulenga vitu vinavyotembea, zitaimarisha mashambulizi na kupunguza idadi ya raia wanaoweza kuwa wahanga.

Lakini wapinzani walisema hatua ya Uingereza kujiingiza katika anga ya Syria iliyojaa madege ya kivita ya mataifa mengine hakutaleta mabadiliko makubwa na kusema mpango wa waziri mkuu Cameron unapuuza hali halisi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

Uingereza tayari ilikuwa na ndege nane za Tornado na ndege zisizo rubani katika muungano unaoongozwa na Marekani unaoyashambulia maeneo ya kundi la Dola la Kiislamu nchini Iraq na itatuma ndege zaidi.

Mwandishi:Josephat Charo/RTRE/AP/AFP

Mhariri:Daniel Gakuba