Uingereza na Umoja wa Ulaya kurejea mezani
6 Desemba 2020Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen na waziri mkuu wa Uingereza Borris Johnson walifanya mazungumzo kwa njia ya simu siku ya Jumamosi na kuwaagiza wajumbe wao kuendelea na mazungumzo katika jaribo la mwisho la kumaliza tofauti zilizoko.
"Tofauti kubwa bado zimesalia", walisema viongozi hao katika taarifa ya pamoja baada ya mazungumzo ya njia ya simu kutathmini uhusiano wa baadae wa Uingereza na Umoja wa Ulaya.
Pande zote zimekiri kwamba muda unayoyoma wa kufikia makubaliano kabla ya kipindi cha mpito kumalizika mwishoni mwa mwaka huu. Viongozi hao wawili wamegusia pia maendeleo yaliyopatikana katika maeneo kadha lakini bado kuna mgawanyiko katika suala la haki za uvuvi. Jonhson na Von der Leyen wamedai kuwa " hakuna makubaliano yanayowezekana ikiwa tofauti juu ya masuala matatu muhimu ya utawala, uvuvi na kanuni za ushindani hayatapatiwa ufumbuzi".
"Hii ni kete ya mwisho ya mchezo", kilisema chanzo kimoja cha Uingereza kilicho karibu na timu ya mazungumzo. "Kuna mpango mzuri unaofaa kufikiwa ambao utafanya kazi kwa pande zote mbili, lakini hili litatokea endapo tu Umoja wa Ulaya utakuwa tayari kuheshimu kanuni za msingi za uhuru na udhibiti".
Kiongozi wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya kwenye mazungumzo na Uingereza Michel Barnier, amesema mazungumzo ya Jumapili na mwenzake wa Uingereza David Frost yatadhihirisha kama makubaliano yanaweza kufikiwa. Mazungumzo baina ya pande hizo mbili, yalisimama siku ya Ijumaa baada ya matumaini ya makubaliano yaliyokuwepo awali kuyeyuka, huku timu ya Uingereza ikisema kwamba Umoja wa Ulaya umetoa masharti yasiyoendana na uhuru wake na kuonya kwamba mazungumzo yanaweza kumalizika bila ya makubaliano.
Uingereza ilijiondoa Umoja wa Ulaya mnamo Januari 31, lakini bado imesalia katika soko la pamoja na umoja wa forodha hadi Desemba 31 mwaka huu. Kufikiwa makubaliano kabla ya muda huo kumalizika kutatoa uhakikisho kuwa hakuna ushuru katika bidhaa zinazosafirishwa au kuingizwa na pande zote mbili.
Pande zote zinaweza kuathirika kiuchumi, Ikiwa zitashindwa kuafikiana, lakini wachambuzi wa uchumi wanaonelea kuwa uchumi wa Uingereza ndio unaweza kukumbwa na mtikisiko zaidi kwasabbau ya kutegemea biashara na Umoja wa ulaya kuliko upande mwingine.