Uingereza na Ufaransa zailaumu Syria
10 Aprili 2012Uingereza imesema kwamba hakuna dalili zinazoonyesha kwamba utawala wa Syria una nia ya kuufuata mpango wa amani uliopendekezwa na Kofi Annan ambaye ni mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za Kiarabu nchini humo. Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza, Bw. William Hague, amesema kwamba badala yake, Syria imeongeza kiasi cha mashambulizi dhidi ya wapiganaji wanaoupinga utawala wa Rais Bashar al-Assad.
Tamko la Hague linawiana na kauli ya msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Ufaransa, Bernard Valero. Msemaji huyo ameeleza kuwa madai ya Syria kwamba imeanza kuondoa vikosi vyake katika miji yenye migogoro ni uongo mkubwa usiokubalika na kwamba jambo hilo linaonyesha kuwa jumuiya ya kimataifa lazima iingilie kati. Wanaharakati wanaotetea haki za binadamu, wameripoti kuwa badala ya kuondoa vikosi, utawala wa Syria umetuma wanajeshi wengi zaidi katika baadhi ya ngome za waasi, ukiwemo mji wa Rastan uliopo katika mkoa wa Homs. Wanajeshi wa Syria leo wamewaua watu wasiopungua 31. Kati ya hao, 26 waliuwawa katika mashambulizi yaliyofanyika kwenye wilaya za Bayada na Khalidiya mkoani Homs.
Syria kujadiliwa na kundi la G8
Wakati huo huo, Liu Weimin ambaye ni msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, ameitaka Syria kufanya juhudi zaidi katika kuufuata mpango wa amani. "China inatumaini kwamba pande zote zinazopigana zitaheshimu makubaliano ya kusimamisha mapigano na kuondoa wapiganaji ili kuboresha hali iliyoko hivi sasa," alisema Weimin. Jana na leo, waziri mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan alifanya mazungumzo ya kina juu ya Syria alipokutana na mwenzake wa China, Wen Jiabao pamoja na rais wa nchi hiyo, Hu Jintao.
Bernard Valero wa wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa, amesema kwamba suala la Syria litajadiliwa kwa kina katika mkutano wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na pia kwenye kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi nane zenye nguvu zaidi kiuchumi, zinazounda kundi la G8. Kikao hicho kitafanyika wiki hii mjini Washington, Marekani.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/dpa/afp
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman