Uingereza kutoa ushirikiano zaidi kupata katiba ya EU
23 Agosti 2007Viongozi hao aidha walijadilia mkakati mpya wa kuimarisha huduma za afya katika mataifa masikini kote ulimwenguni ili kufikia malengo ya maendeleo ya millennia ya Umoja wa mataifa vilevile jukumu la kijeshi la Ujerumani nchini Afghanistan.
Waziri mkuu huyo alimthibitishia Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kuwa atatoa ushirikiano zaidi katika Umoja wa Ulaya na kueleza kuwa anaamini bunge lake litapitisha hoja hiyo. Chama upinzani cha Conservative vilevile vyama vya wafanyikazi nchini Uingereza vinatoa wito wa kufanywa kura ya maoni ya kitaifa kuhusu katiba ya Umoja wa Ulaya.Vyama hivyo vya wafanyikazi vina ushawishi mkubwa katika chama tawala cha Leba cha Bwana Brown.Mkutano huo ulifanyika mjini London katika afisi za Downing.
Hiyo ilikuwa ziara ya kwanza ya Bi Merkel nchini humo tangu Bwana Gordon Brown kushika wadhifa huo.
Viongozi hao wawili walijadilia vita nchini Afghanistan ambako mataifa yao yanashiriki katika shughuli za kijeshi zinazosimamiwa na NATO.
Waziri Mkuu Gordon Brown alielezea haja ushirikiano wa pamoja katika jamii ya kimataifa kutowapa mwanya wapiganaji wa Taleban kurejea tena madarakani.Kundi la Taleban linapinga serikali ya Afghanistan .
Kwa upande mwingine wachangiaji wa Uingereza wanalaumu Ujerumani kwa kutochukua jukumu kubwa zaidi la kijeshi nchini Afghanistan mfano kushiriki kwenye mapigano pamoja na vikosi vya Uingereza katika jimbo la Helmand kusini mwa nchi hiyo.Eneo hilo linazongwa na ghasia kwa muda mrefu.hata hivyo Bwana Brown alikwepa kuzungumzia suala hilo moja kwa moja na waandishi wa habari.
Kulingana na Kansela Angela Merkel majeshi ya Uingereza na Ujerumani yana majukumu tofauti katika ujumbe huohuo.
Bi Merkel alieleza kuwa nchi yake inachukua jukumu kubwa la kuimarisha polisi wa Afghanistan wanaohitaji huduma hiyo.
Suala jengine walilojadilia ni hatua za dharura ili kupambana na magonjwa katika mataifa yanayoendelea.
Viongozi hao wanapanga kuzindua mkakati wa ushirikiano wa kimataifa wa afya ifikapo tarehe 5 mwezi ujao ili kuimarisha utoaji wa misaada kutoka mataifa tajiri.Mkakati huo unaazimia kupambana na ugonjwa wa Ukimwi vilevile magonjwa mengine yanayotatiza mataifa yanayoendelea ili kupunguza idadi ya vifo vya watoto.
Mkakati huo una lengo la kuzipa msukumo juhudi za kutimiza malengo ya maendeleo ya Milenia ya kuimarisha huduma za afya ifikapo mwaka 2015.Wafadhili watashirikiana pamoja ili kutoa misaada,vifaa vipya aidha mafunzo katika sekta ya afya katika mataifa yanayoendelea.