Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya?
23 Januari 2013Akizungumza bungeni katika hotuba iliyopewa jina la "Uingereza na Umoja wa Ulaya", Cameron ameahidi kwamba kufikia mwaka 2017 Uingereza itaitisha kura ya maoni kuwapa fursa raia wake kuamua ama kubakia au kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya, endapo chama chake cha kihafidhina kitashinda uchaguzi wa mwaka 2015.
Cameron amesema kwamba anatakata kufikia makubaliano mapya juu ya vipengele vya uanachama wa Uingereza kwenye Umoja wa Ulaya na kwamba baada ya kupatikana makubaliano hayo, Waingereza watafanya uamuzi juu ya hatima ya nchi yao kwenye Umoja huo.
"Na baada ya kuafikiana juu ya muundo huo mpya, tutawapa watu wa Uingereza fursa ya kupiga kura ya maoni inayowataka watoe jibu moja rahisi na la mkato tu: ama kubakia kwenye Umoja wa Ulaya wenye vipengele vipya au kutoka moja kwa moja." Amesema Cameron.
Kauli hii ya Cameron inamaliza miezi kadhaa ya shaka kwamba angelitangaza mpango huo wa kura ya maoni kati ya mwaka 2015 na 2018, na pia imepuuzia kitisho kwamba hatua hiyo itadhoofisha matarajio ya kidiplomasia na kiuchumi ya Uingereza na kuitenganisha na washirika wake.
Ufaransa yaionya Uingereza
Tayari Ufaransa imeshaionya Uingereza juu ya hatari ya kuitisha kura hiyo ya maoni kuamua hatima yake kwenye Umoja wa Ulaya. Akizungumza na kituo cha redio cha France Info mara tu baada ya hotuba ya Cameron kumalizika, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Laurent Fabius, amesema "Kura hiyo inaihatarisha Uingereza yenyewe, maana Uingereza nje ya Ulaya itakuwa vigumu."
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu Cameron amesema kwamba Uingereza haitaki kuvunja daraja na kujitenga na ulimwengu, lakini hali ya mashaka ndani ya Umoja wa Ulaya "inazidi kuongezeka kila uchao", na kwa hivyo umefika wakati kwa Waingereza kutoa kauli yao na kulisawazisha moja kwa moja suala la nchi yao na Ulaya.
Uzito wa kauli ya Cameron
Uwezo wa Cameron kuitisha kura hiyo ya maoni unategemea zaidi ushindi wa chama chake cha Kihafidhina katika uchaguzi wa hapo mwaka 2015.
Kwa sasa chama cha upinzani cha Labour kinaongoza kwenye kura za maoni, huku serikali ya mseto wa Wahafidhina na Waliberali ikiongoza kipindi kigumu cha makato ya matumizi kwenye sekta za umma na kujaribu kupunguza nakisi ya bajeti, jambo linachochea hasira za wapiga kura dhidi ya serikali hiyo.
Wachambuzi wa mambo wanasema kwamba ahadi hii ya Cameron inaonekana zaidi kulenga kukiridhisha chama chake, ambacho kimegawika kuhusiana na suala la Umoja wa Ulaya, lakini pia inaweza kukiweka chama hicho kwenye wakati mgumu zaidi kutokana na pendekezo lake la kuwa na uanachama unaoitwa mwepesi wa nchi yake kwenye Umoja wa Ulaya, ambao una kila dalili ya kupingwa na wanachama wengine wa Umoja huo.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Josephat Charo