Uingereza, Iran zasaka muafaka meli ya mafuta
14 Julai 2019Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Jeremy Hunt, alizungumza siku ya Jumamosi (Julai 13) na mwenzake wa Iran, Mohammad Javad Zarif, ambaye alisema alimuhakikishia kuwa "Tehran haitaki kuuendeleza mzozo" kati ya mataifa hayo mawili.
"Nilimuhakikishia wasiwasi wetu ulitokana na wapi mafuta yaliyomo kwenye Grace One yalikuwa yakipelekwa na sio wapi yametokea," aliandika Hunt kwenye mtandao wa Twitter. Grace One ni meli ya Iran ambayo ilikamatwa kwenye eneo la Gibraltar linalomilikiwa na Uingereza siku ya Julai 4.
Maafisa wa Marekani walidai kuwa meli hiyo ya mafuta ilikuwa ikielekea Syria, ikikiuka vikwazo kadhaa vya Umoja wa Ulaya na Marekani.
Hunt alisema Uingereza "ingeliwezesha suala la kuachiliwa kwa meli hiyo" ikiwa wangelihakikishiwa kuwa ilikuwa haielekei Syria, kufuatia utaratibu wa kimahakama kwenye mamlaka za Gibraltar.
Serikali mjini Tehran ilikasirishwa na kukamatwa kwa meli hiyo, na wiki hii Uingereza ilisema kuwa mashua za kijeshi za Iran zilijaribu "kuizuia njia" meli ya mafuta ya Uingereza kwenye Mlango Bahari wa Hormuz.
Hunt alisema Waziri Kiongozi wa Gibraltar Fabian Picardo "alikuwa akifanya kazi nzuri ya kuratibu suala hilo na kuonesha mwelekeo wa Uingereza kulitatuwa."
Iran yathibitisha mazungumzo na Uingereza
Wizara ya nje ya Iran ilithibitisha kupitia mtandao wake kwamba mawaziri hao wawili walizungumza kwa njia ya simu. "Tunatarajia kwamba uchunguzi wa kisheria huko Gibraltar utapelekea hivi karibuni kuachiliwa kwa meli ya mafuta ya Iran," alisema Zarif.
Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Uingereza alisema kwenye mazungumzo yake na Zarif, aliibua pia suala la kufungwa jela kwa raia wa Uingereza mwenye asili ya Iran, Nazanin Zaghari-Ratcliffe, ambapo Zarif alisema "angeliendelea kusaka suluhisho" la suala hilo, ingawa alisisitiza kuwa raia huyo anatumikia kifungo kwa mujibu wa sheria.
"Iran pia inaitarajia Uingereza kuheshimu sheria za Iran na uhuru wa mahakama," alisema waziri huyo wa mambo ya kigeni ya Iran. Kulikuwa na uvumi kwamba huenda Iran ikamuachia Zaghari-Ratcliffe kwa mabadilishano na meli hiyo.
Mwanamke huyo alikamatwa kwa tuhuma za kula njama ya kuipindua serikali kwa kuendesha mafunzo ya uandishi wa habari wakati alipoitembelea Iran na akahukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa ujasusi na uchochezi.
Mbali ya kuishikilia meli hiyo, mamlaka za Giblatar ziliwakamata pia manahodha watatu na kisha kuwaachia kwa dhamana. Iran ililalamikia kitendo hicho kwa kumuita balozi wa Uingereza mjini Tehran ajieleze, huku ikitoa wito wa meli yake kuachiliwa mara moja.
Hata hivyo, mahakama ya juu ya Gibraltar ilisema kwamba meli hiyo haiwezi kuachiliwa kabla ya angalau tarehe 21 Julai.
dpa/AFP