1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza haijitengi na dunia, Theresa May

27 Machi 2017

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May yuko Scotland kujaribu kuzuia azimio la nchi hiyo kutaka kujitenga na Uingereza, wakati huo huo akiwa anakabiliana na mzozo wa kisiasa huko Ireland Kaskazini.

https://p.dw.com/p/2a3a0
Großbritannien Theresa May Downing Street in London
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Reuters/R. Pohle

Haya yanakuja wakati ambapo waziri mkuu huyo yuko katika siku za mwisho kabla kuzindua mpango wa Uingereza kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya EU.

Huku Uingereza ikiwa bado inajifuta  machozi ya shambulizi la kigaidi karibu na majengo ya bunge huko London wiki iliyopita, May anajiandaa  kuanzisha safari ya nchi yake kujiondoa  kwenye Umoja wa Ulaya wiki hii, hatua itakayoibadilisha Uingereza na Umoja wa Ulaya kabisa.

Mbele ya mazungumzo yake na waziri wa kiongozi wa Scotland Nicola Sturgeon, May, amesema anataka taifa lililoungana zaidi na atapigania haki za kila sehemu ya Uingereza, mara tu mazungumzo ya kuondoka Umoja wa Ulaya yatakapoanza.

Bunge la Scotland linataka kusalia EU

Lakini Sturgeon anataka Scotland isalie katika soko la Ulaya pale Uingereza itakapojitoa na bunge la Scotland, linatarajiwa kuiunga mkono azma yake ya kutaka kura nyengine ya maoni  ya kudai uhuru wake, huku kura hiyo ikitarajiwa kupigwa na bunge siku ya Jumanne.

Schottland Brexit Nicola Sturgeon
Waziri kiongozi wa Scotland Nicola SturgeonPicha: picture alliance/AP Photo/A. Milligan

Katika hiyo ziara yake, May lakini anatarajiwa kusisitiza umoja wa Uingereza na kwamba umoja huo haustahili kufanywa dhaifu. Waziri mkuu huyo amesema mpango wa kutaka kwa mara ya pili kura ya maoni ya uhuru wa Scotland ni jambo linalozua uhasama na inadaiwa huenda akawa mlegevu katika kufanya mazungumzo na Sturgeon kuhusiana na hilo.

"Kwa sasa tunasimama katika hatua muhimu sana kwa Uingereza wakati tunapoanza majadiliano yatakayotuongoza katika ushirikiano mpya zaidi na Ulaya," alisema waziri mkuu huyo, "na nataka niweke wazi kabisa kwamba tunapoelekea katika mchakato huu, haimaanishi kwamba Uingereza itajitenga na Ulimwengu," aliongeza May.

Mazungumzo Ireland Kaskazini yamegonga mwamba

Zaidi ya asilimia 60 ya raia wa Scotland walipiga kura ya kutaka kusalia katika Umoja wa Ulaya katika ile kura ya maoni ya BREXIT, huku asilimia 52 ikiwa walipigia kura kujiondoa katika Umoja wa Ulaya nchini Uingereza na Ireland Kaskazini.

Uwezekano wa mazungumzo ya kujiondoa Umoja wa Ulaya kuvunjika na Uingereza kuondoka patupu, ni jambo linalozidi kuitia wasiwasi jamii ya wakuu wa makampuni ya kibiashara wa Uingereza na wanasiasa wanaounga mkono Umoja wa Ulaya, kutoka pande zote. Mkuu wa majadiliano hayo wa Uingereza Michel Barnier, alionya wiki iliyopita kwamba, iwapo mwafaka hautopatikana basi kutakuwa na msongamano katika bandari ya Dover, safari za ndege kuingia na kutoka Uingereza zitaathirika na usafirishaji wa bidhaa za nyuklia utasimamishwa.

London Pro Europa Demonstration
Waandamanaji mjini London wanaopinga BREXITPicha: Getty Images/AFP/D. Leal-Olivas

Huku hayo yakiarifiwa, mazungumzo ya kuutatua mzozo wa kisiasa wa Ireland kaskazini yamegonga mwamba na haya ni kulingana na chama cha Sinn Fein, ingawa Uingereza ina matumaini kwamba serikali ya muungano inaweza kuundwa  kabla muda wa mwisho Jumatatu.

Chama cha Sinn Fein kinachowawakilisha Waireland Wakatoliki na kile cha Democratic Unionist Party DUP kinachowawakilisha Waprotestanti, vilipewa hadi saa tisa saa za London, Jumatatu kuelewana, la sivyo uamuzi wa moja kwa moja kutoka London utolewe.

Mwandishi: Jacob Safari/AFP/DPA

Mhariri: Yusuf Saumu