Uhusiano wa wakimbizi na waturkana waimarika nchini Kenya
18 Agosti 2017Kilimo hicho ni sehemu ya mradi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii unaogharimu zaidi ya dola milioni 17 katika eneo hilo. Unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia mfuko wa hazina wa dharura kwa ajili ya Afrika na kutekelezwa kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Turkana na mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa.
Mradi huo wa miaka 14 unaokamilika mwaka 2030 unalenga kuimarisha hali ya maisha ya wakimbizi kupitia kilimo, na pia kuwasaidia kuungana na jamaa zao. Kulingana na umoja wa mataifa, mradi huu ni wa kwanza kuanzishwa nchini Kenya.
Augustine Murenzi, ni mmoja kati ya wakimbizi wanaojihusisha na kilimo. Shamba lake dogo liko nyuma ya kibanda chake katika kambi ya wakimbizi ya Kalobeyei iliyo katika kaunti ya Turkana, kaskazini magharibi mwa Kenya.
Vijishamba hivyo vidogo vina upana wa mita 5 hadi 6 na wakulima wanatumia mfumo wa matuta yaliozama kuendeleza kilimo chao. Mfumo huo unaiwezesha ardhi kuhimili maji kwa muda mrefu na hivyo kuyafanya mazao yakue vizuri.
Mkulima mwengine Bi. Rose Ibalu mkimbizi kutoka Sudan Kusini anasema, yeye hutumia majitaka kumwagilia mazao yake ya sukuma wiki na Bamia. Familia yake hupokea dola 14 kwa mwezi kutoka kwa umoja wa mataifa kwa ajili ya kujikimu kwa chakula na fedha hazitoshelezi mahitaji ya familia yake yenye watoto 7 na yeye mwenyewe. Bi Ibalu anasema tegemeo lake kubwa ni katika kijishamba chake hicho kidogo.
Murenzi na mkimbizi mwengine kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo wamesema kutokana na kupokea fedha chache wamekuwa wanabadilishana mazao yao na jamii katika eneo hilo kwa ajili ya kupata m´kaa.
Tegemeo la wakimbizi
Baadhi ya wakimbizi wanalalamika juu ya uhaba wa maji, hatua ya kupima maji ambayo ilianzishwa na shirika la wakimbizi la umoja wa mataifa UNHCR. Shirika hilo la umoja wa mataifa lilichukua hatua hiyo baada ya kugundua kwamba baadhi ya wakimbizi wanatumia maji safi kumwagilia mashamba yao. Humphrey Emuria ambaye ni afisa mwandamizi wa kilimo katika eneo la Turkana magharibi amesema chakula kinachozalishwa na wakimbizi wa Kalobeyei kinasaidia kupunguza gharama za maisha ya kila siku kwa wakimbizi hao pamoja na jamii ya Waturkana.
Turkana ni mojawapo ya maeneo yaliyo na uhaba mkubwa wa mvua na hivyo basi eneo hilo linahitaji mbinu za kuvuna maji ya mvua kama vile visima, pamoja na sehemu za kuhifadhia maji chini ya ardhi. Lakini njia zinazotumika katika kilimo kama matuta yaliyozama na kilimo cha umwagiliaji zinawasaidia wakimbizi kutumia maji yaliovunwa kwa ajili ya kuendeleza kilimo.
Wanakijiji wa Turkana wanaojumuika pamoja na wakimbizi katika mpango huu wa kilimo wanapata mafunzo ya kilimo cha mtama kwa kutumia mbinu ya kujaza mchanga mbele ya eneo linalolimwa zao hilo. Mbinu hiyo inahifadhi maji ya mvua na baadaye maji hayo hutiririka polepole hadi kwenye mimea. Zao la mtama linapokuwa tayari huvunwa na baadaye wakulima wanauza mazao yao kwa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO. Shirika hilo husaga mtama huo na baadaye unga wa mtama hutumika kama lishe kwa wakimbizi.
Hapo kabla jamii za Wakenya katika eneo hilo hazikutaka kujihusisha na wakimbizi kutokana na unyanyapaa unaotokana na neno wakimbizi, lakini siku hizi wakimbizi wanaonekana kama washirika wa kibiashara, jambo linalosaidia kuleta maelewano mazuri katika jamii.
Mwandishi: Fathiya Omar/Reuters
Mhariri:Josephat Charo