1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhusiano wa Korea Kaskazini na Ujerumani Mashariki ya zamani

Miraji Othman5 Novemba 2009

Korea Kaskazini ilivosaidiwa na iliokuwa Ujerumani Mashariki

https://p.dw.com/p/KOuk
Lango la Brandenburger Novemba 9, 1989, wakati Ukuta wa Berlin ulipoporomokaPicha: picture alliance/dpa

Korea Kaskazini ni nchi iliojitenga kabisa duniani. Mtu hawezi kusafiri kwa uhuru katika nchi hiyo na pia ni vigumu kwa urahisi kuwa na mawasiliano na raia wa Korea Kaskazini. Lakini hali ilikuwa vingine hapo kabla. Mwishoni mwa miaka ya hamsini na mwanzoni mwa miaka ya sitini ni kipindi ambapo kulikuweko uhusiano wa karibu baina ya Wakorea na Wajerumani. Wakati huo Korea Kaskazini na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani ziliungana katika urafiki wa kisoshalisti. Vipi urafiki huo ulivokuwa na nini kilichopatikana kutokana na uhusiano huo?

"Nasema, kweli nchi hiyo ni nzuri na watu wake ni wachapa kazi, wenye akili, wenye urafiki na wacheshi."

Muziki huo wa Korea ukipigwa, Renate Hong alionesha picha alizopiga Korea Kaskazini. Ni mwaka mmoja tangu alipoizuri nchi hiyo, na kwa miaka 46 alipigania aifanye ziara hiyo. Huko Korea Kaskazini anaishi Hong Ok Guen, baba wa watoto wake wa kiume. Alijuwana naye mwishoni mwa miaka ya hamsini pale walipokuwa wakisoma mjini Jena, hapa Ujerumani.

"Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani ilikuwa haina kabisa mafungamano na nchi za nje. Kwa sisi tulihisi Korea Kaskazini ni nchi nzuri, licha ya kwamba ni nchi ya mbali iliokuwa na mvutio maalum kwetu. Na kuna sababu nyingine: kwa vile tuliingiliana na wanafunzi wa kigeni, tuklifikiri kwamba nasi tutaweza kutoka nje."

Renate na Hong Ok Guen waliowana, japokuwa jambo hilo lilikuwa rasmi haliruhusiwi. Na baada ya kuzaliwa mtoto wao wa kwanza mambo yalikuwa si rahisi, anaelezea Renate aliye sasa na umri wa miaka 72.

Ok Guen alikwenda kusoma katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani kwa vile Korea Kaskazini wakati huo ilihitaji sana mafundi wa kazi. Baada ya Vita vya Korea nchi hiyo ilikuwa chini kabisa. Licha ya kuwapa mafunzo mafundi wa Ki-Korea Kaskazini hapa Ujerumani, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani pia ilituma zaidi ya wafanya kazi wa mikono, wapiga ramani za majumba, wapangaji wa miji na wahandisi 450 hadi Korea Kaskazini.

Mwaka 1961, muda mfupi kabla ya kujengwa Ukuta wa Berlin, raia wote wa Korea Kaskazini walimariwa na serekali yao warejee nyumbani. Wanafunzi 350 iliwabidi warejee nyumbani, akiwemo pia mume wa Renate. Mkewe aliyekuwa mja mzito wa miezi mitano pamoja na mwanawe wa kiume iliwabidi wabakie Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani.

Hong Ok Guen aliajiriwa katika kiwanda cha kemikali huko Hamhung. Miaka mitatu alikuwa anamwandikia barua mkewe. Baadae kukawa kimya; hadi mwaka jana pale utawala wa Korea Kaskazini ulipowaruhusu Renate Hong na watoto wake kwenda kumuona Hong Ok Guen. Renate baadae alisema:

"Baada ya wanangu kupata nafasi ya kujuwana na baba yao, natamani kwamba uhusiano uwe wa kawaida kabisa, kama vile mtu anavoishi hapa Ulaya au katika nchi nyingine za kidemokrasia. Sijuwi, mimi na umri sasa wa miaka 72, kama mimi nitaweza kuishi kuiona hali hiyo, lakini natamani watoto wangu waishi kuiona hali hiyo."

Mwandishi: Rebecca Roth/ Othman, Miraji/ZP

Mhariri: Mohammed Abdulrahman