1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhusiano wa Israel na Sudan Kusini watiliwa shaka

13 Septemba 2016

Kuendelea kwa mapigano nchini Sudan Kusini kunabua maswali kuhusu mpango mpya wa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netenyahu wa kuimarisha mahusiano na baadhi ya nchi za kiafrika

https://p.dw.com/p/1K18M
Baadhi ya Raia wa Sudan KusiniPicha: Getty Images/AFP/Stringer

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekuwa akitafuta ushirikiano na nchi mbali mbali za kiafrika ikiwa ni katika juhudi ambazo anasema zitasaidia kupunguza makali ya juhudi za kidiplomasia za wapalestina dhidi ya Israel Katika Umoja wa Mataifa.

Kupitia kwa msemaji wa wizara ya mambo ya nje,Israel imesema inaridhishwa na jinsi nchi hiyo inavyofufua mahusiano yake na nchi nyingi za kiafrika na kwa Israel haina mpango wa kuingilia mambo ya ndani ya nchi hizo

Wakosoaji wanasema uhusiano huu mpya wa waziri mkuu wa Israel kutembelea baadhi ya mataifa ya afrika mwezi julai mwaka huu ni wa kutia shaka na haukuzingatia rekodi kuhusu masuala ya haki za binadamu katika mataifa hayo

Madai hayo yanaibuliwa kufuatia uhusiano wa karibu kati ya Israel na Sudan kusini ambayo imetumia majeshi ya Israel na vifaa vya kiuchunguzi kufuatilia mienendo ya wapinzani huku wakosoaji wakiikosoa Israel na kusema kuwa sera yake ya kimataifa ya uuzaji wa silaha imekosa uwazi na usimamizi kutokana na kutokufuatilia malengo ya nchi inayonunua silaha hizo

Israel Ministerpräsident Benjamin Netanjahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Sultan

Ripoti ya umoja wa mataifa iliyotolewa mwez Januari inasema kuwa Vifaa vya kiuchunguzi vya Israel vimekuwa vikitumiwa na wanaijelijensia wa Sudan Kusini kufuatilia mawasiliano ya wapinzani wa Serikali, mbali na hilo ripoti hiyo pia inaonyesha baadhi ya silaha za Israel zilikuwa zimezagaa kwa wingi nchini humo kabla ya kuanza kwa mapigano

Israel ilikuwa ni nchi ya kwanza kutangaza kuitambua Sudan kusini kama taifa huru mwaka 2011 na baadae Salva Kiir kutembelea Israel mwezi mmoja uliofuata, kwa miaka mingi sasa Israel imeitazama Sudan Kusini kama nchi ambayo inaweza kushirikiana nayo

Siku chache kabla ya kuanza tena kwa mapigano nchini humo Netanyahu alitembelea mataifa manne ya afrika ambayo ni Ethiopia, Uganda, Kenya na Rwanda ziara ambayo ililenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia dhidi ya Palestina ikiwa ni ziara yake ya kwanza kwa mafaifa yaliyo kusini mwa jangwa la sahara

Kikao cha Netanyahu na baadhi ya wakuu wa nchi za Afrika

Katika ziara hiyo Netenyahu alifanya kikao na baadhi ya viongozi ikiwemo kiongozi wa Sudan Kusin Salva Kiir na wengine, wengi wao wakiwa ni wale ambao wanashutumiwa na waangalizi kwa uvunjifu wa haki za binadamu

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta aliwahi kufikishwa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC kwa makosa dhidi ya ubinadamu yaliyotokana na ghasia zilizozuka baada ya uchaguzi mwaka 2007 hadi 2008 madai ambayo baadae yalifutiliwa mbali n mahakama hiyo ya ICC.

Rais wa Uganda Yoweri Museven ambaye amekuwa kiongozi wa nchi hiyo kwa miaka 30 sasa na anakusudia kuongeza muda wa kuendelea kuwa madarakani, upande mwingine Rais wa Rwanda Paul Kagame anashutumiwa kwa uvunjaji wa haki za binadamu katika nchi jirani ya jamhuri ya kidemocrasia ya Congo huku akikosolewa na baadhi ya makundi ya haki za binadamu kuwa utawala wake ni wa kidikteta

Tangu Sudan kusini iingie katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013 watu elfu 50 wamefariki na wengine milioni mbili wamepoteza makazi yao , Mwezi Julai maelfu walifariki kutokana na mapigano yaliyoibuka katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba

Baadhi ya walioshuhudia waliohojiwa na vyombo vya habari wanasema majeshi ya Sudan Kusini yalivamia katika hoteli moja na kumuua mwandishi wa habari huku wakiwalazimisha watu wengine kutazama, kuwabaka wanawake wa kigeni na pamoja na kuiba bidhaa.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/AP

Mhariri:Yusuf Saumu