Uhusiano wa biashara kati ya China na Ghana waimarika
31 Julai 2008Zao jipya katika orodha hiyo ni kakao.Mwaka huu Ghana inatazamia kuiuzia China tani 6,500 baada ya serikali ya Ghana kutangaza makubaliano ya kuzidisha uzalishaji wa kakao ili China iweze kupatiwa kakao zaidi.Pato la biashara hiyo litasaidia ujenzi wa mtambo utakaozalisha nishati kwa nguvu za maji huko Bui kaskazini-mashariki ya mji mkuu Accra.
Biashara kati ya nchi hizo mbili imezidi kuimarika miaka ya hivi karibuni lakini ni China inayonufaika zaidi.Licha ya manufaa ya mradi huo wa Bui,baadhi ya Waghana wana hofu kuwa China peke yake inafaidika tangu masoko ya barani Afrika kuwa huru zaidi.Wananchi hao hasa wanachukizwa na msimamo wa China kuelekea Ghana huku bidhaa rahisi kutoka China zikizidi kuenea kila kona.Takriban kila nchi ya Kiafrika imefungua milango yake kwa bidhaa rahisi zinazotoka China.
Hivi karibuni Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Kakao ya Ghana,Isaac Osei alipozungumza kwenye mkutano wa Biashara na Maendeleo wa Umoja wa Mataifa-UNCTAD uliofanywa Ghana alisema,jitahada za Ghana kuendeleza biashara ya kakao pamoja na madola yanayoinukia kiuchumi,kama vile China na India huvunjwa nguvu. Amesema,nchi zilizoendelea katika uzalishaji wa bidhaa hiyo kama vile Ghana na Ivory Coast hutozwa ushuru mkubwa zaidi wa forodha kulinganishwa na zile ambazo hazikuendelea hivyo katika sekta hiyo kama vile Benin,Guinea,Togo au Uganda.
Kwa upande mwingine,mtaalamu wa uchambuzi wa bidhaa mjini London,Alfred Niemann amesema,China inapaswa kufungua zaidi masoko yake inapofanya biashara na nchi masikini zinazoendelea. Amesema,si haki kwa China kuzuia bidhaa kutoka nje kuingia kwake wakati ikitumia mazingira ya biashara huru, kueneza bidhaa zake rahisi katika nchi masikini hasa barani Afrika.
Lakini yadhihirika kuwa Ghana imeshajipangia mwongozo wake na inatazamia kutimiza lengo la kuzalisha hadi tani milioni moja za kakao ifikapo 2010.Kwa hivyo sasa ndio inatafuta masoko zaidi kwa zao hilo.Na China ni soko linalotupiwa jicho.Uhusiano wa biashara ukiendelea kuwa mzuri,Ghana bila shaka haitopata shida kuuza nje kakao zaidi mpaka itakapokuwa na mitambo yake yenyewe kuzalisha bidhaa zingine kutoka kakao.
Nchini Ghana,kiwanda cha kakao kinaajiri kama watu milioni moja katika wilaya sita mbali mbali zinazolima kakao.Kiwanda hicho kinachangia sehemu kubwa ya pato la serikali.Kwa mfano,mwaka jana kilimo cha kakao kiliipatia Ghana kama Dola bilioni 1.2.