1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhusiano baina ya China na Uingereza

30 Desemba 2009

China na Uingereza zabadilishana lawama

https://p.dw.com/p/LHJJ
Waziri mkuu wa Uengereza, Gordon Brown

Kuuliwa kwa mshukiwa wa Kiingereza, Akmal Shaikh, nchini China kwa tuhuma za ulanguzi wa madawa ya kulevya hapo jana, sasa kumechipua sitofahamu ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Familia ya marehemu Shaikh sasa inailekezea kidole cha lawama Uingereza kwa kushindwa kuokoa maisha ya mshukiwa.

Tukio lililogonga vichwa vya habari kimataifa la kuuawa kwa mshukiwa wa Uingereza nchini China kwa madai ya ulanguzi wa madawa ya kulevya bado linaendelea kutifua kivumbi.

Sasa Uingereza inadai kuwa China iliihujumu kwa kutokubali kufanya mazungumzo kabla ya kutekeleza mauaji.

Wadadisi wa kisiasa wanadokeza kuwa kifo cha Akram Shaikh kimekuwa chanzo cha kukwaruza upya uhasama kati ya Uingereza na China ambao una mizizi kutoka katika enzi za ukoloni.

Kupuuzwa kwa juhudi za madaktari wa Uingereza kutathmini hali ya afya ya mshukiwa, ndiko kunaonekana kuwakera zaidi Waingereza.

Zaidi ya haya Uingereza inadai kuwa haikujulishwa kuwa raia wake alikuwa amekamatwa; mwaka mmoja tangu atiwe mbaroni.

China, kwa upande wake, imesisitiza kuwa inatekeleza shughuli kwa mujibu wa sheria zake wala sio kwa shinikizo za nchi za ulaya.

Jambo ambalo limezua mjadala ni kwamba ikiwa Wachina wanawauwa washukiwa wao, mbona mgeni asamehewe kwa sababu ni raia wa moja ya nchi zenye ushawishi duniani!!

Kulingana na takwimu za shirika la kutetea haki za kibinadamu , Amnesty International; mwaka wa 2008, China ndio ilikuwa ikiongoza zaidi kwa matukio 1700 ya washukiwa kuuawa, kisha zaidi ya 300 kule Iran na pia takriban washukiwa wengine 111 katika mikoa kadhaa ya Marekani.

Ni dhahiri shahiri kwamba uamuzi wa ngazi ya juu unaotolewa na majaji wa mahakama ya rufaa nchini China, hushinikizwa na viongozi wakuu katika chama cha Kikomunisti, hivyo kuwa vigumu zaidi kubatilishwa.

Kati ya malalamiko yanayolimbikiziwa China sasa, ni kiburi cha kidiplomasia katika misingi kuwa inaweza kujitegemea, kiuchumi.

Waziri wa mazingira wa Uingereza, Ed Milliband, awali aliwahi kugusia kumea pembe huku kwa China na ambao ulihusishwa pakubwa na tuhuma za China kushirikiana na nchi zingine kutatiza makubaliano na uiano katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa kule Copenhagen.

Waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, alisisitiza kuwa kuuawa kwa shaikh hakukufaa kabisa na kulionekana kuharakishwa bila misingi thabiti ya majadiliano. Naye waziri wa maswala ya nje wa Uingereza , Ivan Lewis, alichangia akisisitizwa kuwa China imeshindwa kuzingatia ahadi za kimataifa za kulinda haki msingi ya kibinadamu.

China ilipuuzilia mbali madai kuwa mshukiwa alikuwa na matatizo ya kiakili na kuwa alistahili kuuawa ili iwe funzo kwa washukiwa wengine wenye nia kama yake ya ulanguzi wa madawa ya kuleva. Akmal shaikh, ambaye ni Muislamu, alitarajiwa kufanyiwa mazishi kulingana na utaratibu wa dini kabla ya masaa 24.

Mwandishi: Peter Moss/AFP

Mhariri: Miraji Othman