1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhuru na Raila: Misimamo mikali kila upande

21 Februari 2018

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, alipoandaa kiapo cha yeye kutawazwa kama ‘rais wa watu' mjini Nairobi tarehe 30 Januari, baadhi ya watu walikiona kitendo hicho kama cha kipuuzi.

https://p.dw.com/p/2t6VR
Kenia symbolische Vereidigung Raila Odinga
Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/B. Jaybee

Uhuru vs Raila: Misimamo mikali kila upande

‘Kiapo' hicho hakikuwa na nguvu yo yote ya kisiasa nchini na wala hakikumpa Raila uwezo wa kumtikisa ‘rais wa kweli' aliyeketi Ikulu ya Nairobi, Uhuru Kenyatta. Wengi walikiona kama kitendo cha mtu aliyezidiwa na mashauzi na mbwembwe lakini sasa inaanza kuonekana kwamba athari za kitendo hicho ‘cha kipuuzi' ni kubwa kuliko ilivyodhaniwa anasema mwandishi habari mkongwe kutoka Daresalam Jenerali Ulimwengu katika uchambuzi wake kuhusu siasa za Kenya.

Kwanza, tukio hilo la ‘mzaha' lilihudhuriwa na hadhara kubwa kupita kiasi, takriban watu milioni moja, ambalo si jambo la kubeza. Pili, kinyume cha hofu iliyokuwapo kuhusu hali ya utulivu wa halaiki kama hiyo, utulivu ulitamalaki, pamoja na kwamba askari polisi hawakutanda mahali hapo. Tatu, na muhimu zaidi, ni kwamba umati huo ulionekana kumshangilia Raila Odinga, kiongozi wa muungano wa Nasa, kama kiongozi wao mkuu.

Uzito wa dondoo hii ya tatu ilishadidiwa na kutokuwapo kwa viongozi wengine wa Nasa, Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula. Baada ya tukio, wote watatu walijaribu kutoa sababu za kutoonekana, lakini ilikuwa wazi kwamba waliogopa kuonekana kwenye tukio hilo. Kutotokea kwao kulimsaidia Raila kujikusanyia uaminifu wa hadhira kubwa yote ile bila kulazimika kugawana umaarufu na upendo wa halaiki na mtu ye yote mwingine, na Raila alionekana kuifurahia hali hii kwa kiasi kikubwa.

Miguna Miguna alikimbizwa uhamishoni Canada

Hata hivyo, tukio hili la ‘kiapo' lingeweza kubakia kama tamthilia tu iwapo Uhuru na utawala wake wa Jubilee wangekipuuza badala ya kukichukulia kama suala la uhaini na kuanza kuchukua hatua za ukandamizaji wa uhuru wa wale walioonekana kama waliomsaidia Raila katika kufanikisha tamthilia yake.

Kenia Uhuru Kenyatta Wahlsieger
Rais Uhuru Kenyatta wa KenyaPicha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Miguna Miguna, anayejiita ‘Jemadari wa Harakati za Ukombozi wa Kenya' (NRMKe), ambaye ndiye aliyemlisha ‘kiapo' Raila, alisombwa na wanausalama wa serikali, akakimbizwa uwanja wa ndege akakimbizwa uhamishoni nchini Canada ambako ni raia na mwanasheria . Aidha serikali ilivifungia vituo kadhaa vya televisheni visionyeshe tukio la ‘kiapo' na ikakataa kuvifungulia hata baada ya mahakama kuiamuru ivifungulie. Pia, serikali ilizifuta hati za kusafiria za viongozi kadhaa wa Nasa, hivyo kuwafanya wasisafiri nje ya nchi.

Raila na washirka wake wamelaani hatua hizi za serikali ya Uhuru kwa kusema zinairudisha Kenya kwenye enzi za udikteta wakati wa utawala wa Rais Daniel arap Moi. Mwandishi wa safu ya maoni mjini Nairobi, Rasna Warah, ameandika katika The Citizen la Tanzania  akimuonya Uhuru kujichunga asije akairudisha Kenya kwenye zama hizo za kiza. ‘Watu wanajiuliza ni nini serikali itafanya sasa, kufungua upya vyumba vya kutesa watu katika Jumba la Nyayo?'

Kampeni za kususia biashara na bidhaa za viongozi wa Jubilee zaendelea

Inaonekana kutakuwapo na hatua zaidi za upinzani dhidi ya serikali ya Uhuru. Mikutano mikubwa ya hadhara imepangwa kote nchini, na imependekezwa kwamba baada ya mikutano hii, ‘mkutano mkuu wa kitaifa' utakutana mjini Nairobi mwishoni mwa mwezi na kupitisha maazimio yatakayowasilishwa kwa wananchi kwa ajili ya kura ya maoni.

Kenja Oppositionsführer Raila Odinga
Raila Odinga alijiapisha kama RaisPicha: DW/Kiswahili

Kiongozi wa mikakati wa Nasa, David Ndii amesema, ‘Lengo letu ni kuona mchakato wa mkutano mkuu wa kitaifa ukituongoza hadi kufanya uchaguzi wa rais utakaofanyika chini ya sheria na kanuni mpya za uchaguzi kabla ya mwisho wa mwezi Agosti 2018.

Wakati huo huo, kampeni zinaendelea kususia biashara na bidhaa zinazojulikana kuhusiana na viongozi wa Jubilee, na jambo la kutisha linalosikika siku hizi ni lile la ‘kujitenga' kwa sehemu za Kenya na vilevile  wazo la kupokezana kwa madaraka ya serikali miongoni mwa majimbo ya nchi hiyo.

Ni dhahiri kwamba Kenya ni nchi iliyogawanyika vibaya, na ni wazi kwmaba vinahitajika vichwa vilivyotulia kuisaidia kurudi katika mwafaka, utangamano na amani. Tatizo ninaloliona ni kwamba pande zote mbili zinazokinzana zinaongeza ukali wa misimamo yao badala ya kuipoza. Kwa bahati mbaya, hata Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) haionekani kama inao utashi au uwezo wa kuchukua hatua za kuwasaidia Wakenya wajikwamue kutokana na zahama hii, ambayo inaweza kusababisha majanga makubwa.

Mwandishi:Jenerali Ulimwengu

Mhariri:Saumu Mwasimba