1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhuru Kenyatta ndiye rais mpya wa Kenya

30 Oktoba 2017

Uhuru Kenyatta ndiye rais mteule wa taifa la Kenya baada ya kuzoa kura milioni 7.4 ya kura zote zilizopigwa kwenye  uchaguzi mpya  wa urais.

https://p.dw.com/p/2mksv
Kenias Staatschef Kenyatta gewinnt Präsidentschaftswahl
Picha: Picture-Alliance/dpa/AP/S. A. Azim

Tume ya Kusimamia uchaguzi na mipaka imesema kuwa wapiga kura milioni 7.6 walijitokeza kupiga kura wakiwakilisha asilimia 42.3 Tume hiyo imesema kuwa matokeo kwenye majimbo manne ambayo hayakujumuishwa kwenye mchakato wa uchaguzi kufuatia machafuko hayana athari kubwa kwenye matokeo ya kura zilizopigwa.

Mwenyekiti wa Tume hiyo Wafula Chebukati amesema kuwa uchaguzi huo uliendeshwa kwa njia huru, haki na ya kuaminika. Kenyatta ataapishwa baada ya majuma mawili iwapo hakuna kesi itakayowasilishwa kwenye mahakama ya Juu kupinga uteuzi wake. Shisia Wasilwa anaripoti kutoka nairobi.

"Kabla ya uchaguzi kupigwa nilikuwa nimeridhika kuwa tulikuwa tumefanya kila kitu kilichohitajika kufanya, wakati huu hakukuwa na vitisho ama muingilio kutoka kwa mtu yeyote," alisema Chebukati.

Uhuru Kenyatta aliwashinda wagombea wengine sita kwenye uchaguzi ambao alitarajiwa kushinda kwa urahisi baada ya kushindana na wagombea ambao hawana umaarufu nchini Kenya.

Chebukati anasema amezingatia sheria katika kuendesha uchaguzi

Idadi ndogo ya wapiga ikijitokeza kutekeleza haki yao ya kidemokrasia huku ngome za upande wa upinzani zikisusia uchaguzi wenyewe. Kenya imefanya chaguzi mbili katika miezi miwili, suala ambalo mwenyekiti wa tume ya Kusimamia uchaguzi na Mipaka Wafula Chebukati amesema limekuwa changamoto.

Kenia Wahlwiederholung | Chef der Unabhängigen Wahlkommission (IEBC) Wafula Chebukati
Mwenyekiti wa IEBC Wafula ChebukatiPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Abdul Azim

Hata hivyo Chebukati anashikilia kuwa amezingatia sheria na maadili kwenye mchakato mzima wa marudio ya uchaguzi huu ambao baadhi ya waangalizi wametaja kuwa ulikuwa huru na wa haki hivyo kuwataka wakenya kutangamana na kujenga taifa, licha ya kunukuliwa awali akisema kuwa hana uhakika na mazigira ya uchaguzi huru na wa haki.

Septemba mosi, mahakama ya Juu ilibatilisha uchaguzi wa urais ambao ulifanywa tarehe nane mwezi Agosti na kuagiza uchaguzi mpya ufanywe.

Mahakama hiyo iliamua kuwa uchaguzi huo ulikiuka sheria na katiba. Kwa mujibu wa matokeo yaliotangazwa na Tume wakati huo. Rais Uhuru Kenyatta alikuwa amemshinda kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa kura milioni 1.4.

Hata hivyo Odinga alijiondoa baada ya masharti yake kutozingatiwa na Tume hiyo. Tume hiyo imefanya uamuzi huo licha ya majimbo manne ya Nyanza kutoshiriki kwenye uchaguzi huo. Matokeo ya leo yametoka kwenye vituo 266 vya kupigia kura kati ya vituo 290.

Tume ilifanya mageuzi kabla uchaguzi

Naibu wa mwenyekiti wa Tume ya Kusimamia Uchaguzi  Consolata Nkatha alielezea kuridhika kwao, "Kama inavyaogizwa kufanyika kwa marudio ya uchaguzi, tumeridhika kuwa katika maeneo ambayo uchaguzi uliahirishwa, matokeo ya uchaguzi hayatakuwa na athari kubwa kwa matokeo ya urais." alisema Nkatha.

Kenia Ezra Chiloba Leiter der Wahlkommission
Afisa Mkuu wa IEBC Ezra Chiloba alitakiwa na upinzani kujiuzuluPicha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Mageuzi ambayo tume ilifanya kabla ya uchaguzi ni pamoja na kuongeza mitambo ya kutuma matokeo ya uchaguzi, kuhusisha mawakala wa vyama mbali mbali kwenye mchakato mzima wa uchaguzi, huku maafisa wake wakipewa mafunzo ya kutosha.

Hata hivyo rais Uhuru Kenyatta alisusia mkutano ambao alitarajiwa kukutana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga pamoja na mwenyekiti wa Tume hiyo Wafula Chebukati kulainisha masuala tata kabla ya uchaguzi kurudiwa.

Upinzani ulitaka baadhi ya maafisa wa Tume hiyo watimuliwe afisini hali ambayo baada ya vuta nikuvute  ya muda mrefu, afisa mkuu mtendaji wa Tume hiyo Ezra Chiloba alitangaza anachukua likizo ya wiki tatu.

Upande wa upinzani ulitisha kutangaza Odinga mshindi, iwapo Chebukati angemtangaza Kenyatta mshindi. Hilo linasubiriwa kwa sasa. Huku macho yote ya jumuiya ya Afrika Mashariki yakilenga demokrasia ya taifa Kenya, wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa masuala tata kama vile ya ukabila yanastahili kujadiliwa na kila mmoja mkenya ahusishwe kwenye serikali ili ahisi ni sehemu ya taifa.

Mwandishi: Shisia Wasilwa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman