1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uholanzi yawaadhiri mabingwa watetezi Uhispania

14 Juni 2014

Hakuna mtu aliyetarajia, lakini Wadachi walikuwa hawashikiki na kushambulia kama nyuki dhidi ya wabingwa watetezi wa kombe la dunia Uhispania na kufunga mabao safi 5-1 ambayo yameiweka Uhispania katika njia panda.

https://p.dw.com/p/1CIFn
WM 2014 Gruppe B 1. Spieltag Spanien Niederlande
wachezaji wa Uholanzi wakishangiria baoPicha: Reuters

Ushindi wa Uholanzi wa mabao 5-1 jana Ijumaa usiku(13.06.2014) huku mvua ikinyesha , ilikuwa ni shangwe kwa mashabiki wa Uholanzi waliovalia mashati yao ya rangi ya chungwa katika uwanja wa Arena Fonte Nova, wakati wakisherehekea mmoja kati ya ushindi mnono kabisa kwa timu yao ya taifa ikiwa ni kama mchezo wa marudio wa fainali ya mwaka 2010 ya kombe la dunia nchini Afrika kusini.

Kipigo hicho kwa mabingwa hao watetezi dhidi ya Uholanzi ndio kikubwa zaidi kwa mabingwa watetezi katika kombe la dunia.

WM 2014 Gruppe B 1. Spieltag Spanien Niederlande
Shabiki wa Uhispania haamini macho yakePicha: Dani Pozo/AFP/Getty Images

Uhispania imepata cheo hicho kutoka Ujerumani ambayo baada ya kunyakua ubingwa wa dunia mwaka 1954 ilipoteza mchezo wa kuwania nafasi ya tatu dhidi ya Ufaransa kwa mabao 6-3 katika fainali za mwaka 1958. Kutokana na hayo kipigo dhidi ya Uhispania mjini Salvador Brazil , kilikuwa ni kikubwa kwa mabingwa watetezi katika mchezo wa kwanza.

Mabingwa wengine pia walishindwa

Mabingwa wengine pia wameshindwa katika mchezo wa kwanza , kama vile Ufaransa mwaka 2002 dhidi ya Senegal na Argentina mwaka 1982 dhidi ya Ubelgiji na mwaka 1990 dhidi ya Cameroon.

Michezo yote hiyo ilimalizika kwa kipigo cha bao 1-0 wakati magoli mengi zaidi yaliyofungwa katika mchezo wa kwanza hadi jana Ijumaa ilikuwa ni magoli matatu katika mchezo kati ya Italia na Sweden mwaka 1950 ambapo Sweden ilishinda kwa mabao 3-2.

WM 2014 Gruppe B 1. Spieltag Spanien Niederlande
Iker Cassias mlinda mlango wa UhispaniaPicha: Javier Soriano/AFP/Getty Images

Matokeo ya jana yalikuwa kipigo cha juu kabisa kwa Uhispania katika kombe la dunia tangu walipofungwa mabao 6-1 Julai 13 ,mwaka 1950 dhidi ya wenyeji Brazil.

Hata hivyo Uhispania ina nafasi ya kusonga mbele iwapo itazishinda Australia na Chile katika michezo yake ijayo.

WM 2014 Gruppe A 1. Spieltag Mexiko Kamerun
Mexico wakishangiria bao lao la ushindi dhidi ya CameroonPicha: Reuters

Del Bosque kichwa chini

Kocha wa Uhispania Vicente del Bosque amekataa kumnyooshea kidole mmoja kati ya wachezaji wa kikosi chake na kusema , "haikuwa wakati wa furaha kwetu". Kama mwanamichezo napenda kukipongeza kikosi cha Uholanzi, walituvuruga kabisa kipindi cha pili, ameongeza del Bosque. Tunapaswa kuangalia mbele na kuingia katika mchezo mwingine na kupata ushindi dhidi ya Chile, amemaliza del Bosque.

Kikosi cha kocha wa Mexico Miguel Herrera kiliwagaragaza Simba wa nyika Cameroon kwa bao 1-0 katika uwanja wa Estadio das Dunas jana.

WM 2014 Gruppe A 1. Spieltag Mexiko Kamerun
Mpambano Kati ya Mexico na CameroonPicha: Getty Images

Cameroon ambayo ilichechemea kuelekea nyumbani kutoka Afrika kusini miaka minne iliyopita bila kupata point kutokana na michezo mitatu, inakabiliwa na marudio ya hali hiyo iwapo itashindwa kupata ushindi dhidi ya Chile na Croatia wiki ijayo kabla ya mpambano wao wa mwisho dhidi ya wenyeji Brazil hapo Juni 23.

Cameroon hawakuonesha kabisa makali ambayo waliyaonesha katika mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya Ujerumani wiki mbili zilizopita mjini Mainz.

WM 2014 Gruppe B 1. Spieltag Chile Australien
Wachezaji wa Chile wakishangiria baoPicha: William West/AFP/Getty Images

Kocha wa Mexico Herrera ambaye ametangaza wazi kuwa ana nia ya kuipeleka timu hiyo hadi fainali na kuandika historia , amesema amefurahishwa mno na uchezaji wa kikosi chake dhidi ya Cameroon.

Katika mchezo wa mwisho jana Chile iliisambaratisha Australia kwa kuifunga mabao 3-1, licha ya kuwa Australia ilionesha ujasiri wa hali ya juu katika mchezo huo.

Leo kutakuwa na pambano kati ya Cote D'Ivoire na Japan , halafu jioni ni kati ya Colombia na Ugiriki , England itakwaana na Italia, na Uruguay itapambana na Costa Rica.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe