1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUholanzi

Uholanzi yaomba radhi kwa nchi hiyo kuhusika katika utumwa

19 Desemba 2022

Waziri Mkuu wa Uholanzi, Mark Rutte ameomba rasmi radhi kutokana na nchi hiyo kuhusika katika biashara ya utumwa, akisema utumwa unapaswa kutambuliwa kwa maneno yaliyo wazi zaidi kama ni "uhalifu dhidi ya ubinaadamu."

https://p.dw.com/p/4LBLm
Ukraine Niederlande Mark Rutte
Picha: Andrew Kravchenko/AP/picture alliance

Akihutubia Jumatatu jioni kuhusu historia ya utumwa katika Hifadhi ya Kitaifa huko The Hague, Rutte amesema anaomba radhi kwa niaba ya serikali ya Uholanzi na kutokana na vitendo vilivyofanywa na taifa la Uholanzi.

Rutte ameomba radhi rasmi licha ya kuwepo wito kutoka kwa makundi ya wanaharakati wa Uholanzi na makoloni yake ya zamani, ambao wanadhani msahama huo unapaswa kuombwa mwaka ujao tarehe 1 Julai, wakati wa kumbumbuku ya kumalizika kwa utumwa kwenye makoloni yake ya zamani miaka 160 iliyopita.

Kiongozi huyo amesema hakuna wakati mzuri kwa kila mtu, hakuna maneno sahihi kwa kila mtu, hakuna sehemu sahihi kwa kila mtu. Amesema serikali yake itaanzisha mfuko kwa ajili ya mipango ambayo itasaidia katika kusaidia kukabiliana na athari za utumwa nchini Uholanzi na kwenye makoloni yake ya zamani.

Amsterdam | Nationale Erinnerung an Geschichte der Sklaverei
Kumbukumbu ya kitaifa ya historia ya utumwa Amsterdam, UholanziPicha: Peter Dejong/AP/picture alliance

Wawakilishi wa baraza la mawaziri pia wanatarajiwa kuzungumza katika koloni la zamani la Uholanzi, Suriname huko Amerika Kusini, na vile vile kwenye visiwa sita vya Carribbean, ambavyo bado hadi leo ni milki ya utawala wa Kifalme wa Uholanzi.

Wakati mmoja Uholanzi ilikuwa nchi ya tatu yenye nguvu kubwa ya kikoloni ulimwenguni na iliwafanya takribani watu 500,000 kuwa watumwa katika kipindi cha miaka 200 iliyopita. Wengi wao walitekwa nyara kutoka Afrika Magharibi, wakauzwa na wakalazimishwa kufanya kazi katika mashamba ya Suriname na Antilles. 

Wanaharakti wadai 2023 ndiyo kumbukumbu ya miaka 150

Wanaharakati wanauchukulia mwaka ujao kama kumbukumbu ya miaka 150 kwa sababu watumwa wengi walilazimishwa kuendelea kufanya kazi katika mashamba kwa muongo mmoja baada ya kumalizika kwa biashara ya utumwa.

Utawala wa Kifalme wa Uholanzi ulikuwa mojawapo ya nchi za mwisho barani Ulaya ambazo ziliachana rasmi na biashara ya utumwa mnamo tarehe 1 Julai, mwaka 1863. Mwisho halisi wa utumwa ulikuwa mwaka 1873.

Awali, serikali ya Uholanzi ilionesha masikitiko makubwa kwa historia yake ya kuhusika katika biashara ya utumwa, lakini haikuwahi kuomba msamaha rasmi. Kwa miaka mingi serikali ya Rutte ilikataa kuomba radhi, huku wakati mmoja akisema kuwa tamko kama hilo linaweza kuigawa jamii. Hata hivyo, wabunge wengi wanaunga mkono suala la kuomba radhi.

Niederlande | Sklaverei Mahnmahl in Amsterdam
Mnara wa Kitaifa wa Utumwa ulioko Amsterdam, UholanziPicha: Remko de Waal/ANP/AFP

Tume iliyoteuliwa na serikali ilitangaza mwezi Julai kwamba Uholanzi inapaswa kuomba radhi na kufanya kazi kikamilifu kupambana na madhara yatokanayo na utumwa kama vile ubaguzi wa rangi. Utumwa ulikuwa uhalifu dhidi ya ubinaadamu na serikali ilipaswa kutambua "udhalimu wa kihistoria."

Uholanzi ilijihusisha kwa mara ya kwanza na biashara ya utumwa kupitia Bahari ya Antlantiki mwishoni mwa miaka ya 1500 na kuwa mfanyabiashara mkubwa katikati ya miaka ya 1600. Miji ya Uholanzi ukiwemo mji mkuu, Amsterdam na mji wa bandari wa Rotterdam tayari iliomba radhi kutokana na historia ya kuhusika na biashara ya utumwa.

Mwaka 2018, Denmark iliomba radhi kwa Ghana, ambayo iliitawala kuanzia katikati ya karne ya 17 hadi katikati ya karne ya 19. Mwezi Juni, Mfalme Philippe wa Ubelgiji alielezea ''masikitiko makubwa'' kutokana na unyanyasaji nchini Kongo. Aidha, mnamo mwaka 1992, aliyekuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa John Paul wa Pili, aliomba radhi kutokana na kanisa kuhusika katika utumwa.

(DPA, AFP, AP, Reuters)