1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uholanzi yamaliza katika nafasi ya tatu

13 Julai 2014

Baada ya mchezo kukamilika, ni Uholanzi iliyoshangiliwa na umati wa Brazil. Brazil iliondoka uwanjani kwa kuzomewa, baada ya kichapo kingine kilichohitimisha ndoto ya kutwaa Kombe la Dunia katika ardhi yao

https://p.dw.com/p/1Cbw4
WM 2014 Spiel um Platz drei Brasilien Niederlande
Picha: Reuters

Kampeni ya kusisimua ya Uholanzi ilifikia kikomo kwa ushindi baada ya Robin Van Persie na Daley Blind kufunga magoli ya mapema na kuisidia timu yao kusajili ushindi wa magoli matatu kwa sifuri dhidi ya Brazil na kuibuka mshindi wa tatu. Kocha wa Uholanzi Louis Van Gaal alisema “tunaweza kuangalia nyuma na kusema tulikuwa na dimba lenye mafanikio. Ninajivunia wachezaji wangu”.

Kwa maara ya kwanza, Uholanzi imekamilisha Kombe la Dunia bila kushindwa katika muda wa kawaida, baada ya kupoteza kwa Argentina kupitia penalty katika nusu fainali. Baada ya kumaliza makamu bingwa katika mwaka wa 2010, nafasi ya tatu ndiyo nafasi nzuri zaidi kwa kikosi cha Uholanzi tangu iliposhindwa katika fainali ya 1974 na 1978.

Mashabiki wa Brazil waliwapongeza kwa sauti kubwa wachezaji wa Uholanzi baada ya kupokea nishani zao za shaba, na kunyanyuka kwenye viti vyao kama ishara ya heshima. “Ningependa kuwashukuru watu wote nchini Brazil kwa kutuunga mkono,” Alisema Arjen Robben. “Kwetu ilikuwa njia nzuri ya kumaliza dimba hili. Tulistahili kupata nafasi ya tatu kulingana na namna tulivyocheza. Ni mafanikio makubwa sana.”

WM 2014 Spiel um Platz drei Brasilien Niederlande
Wachezaji wa Brazil walionekana kufedheheka mno wasijue la kufanya baada ya kichapo cha pili mfululizoPicha: Reuters

Kichapo hicho kwa Brazil kiliongeza hali ya kukata tamaa katika dimba hilo kufuatia kichapo cha magoli saba kwa moja ilichokipata kutoka timu ya Ujerumani. Baada ya kipyenga cha mwisho kupulizwa, timu hiyo ilizomewa na karibu mashabiki 70,000 waliofika uwanjani katika uwanja wa taifa wa Brasilia. Ni mara ya kwanza tangu mwaka wa 1940 ambapo Brazil imepoteza mechi mbili za mashindano kwenye ardhi ya nyumbani.

“Ni uchungu sana, sijui hata niseme nini,” alisema Oscar. “Baada ya kichapo kikubwa dhidi ya Ujerumani, leo tulijaribu tuwezavyo kutoka mwanzo kushinda nafasi ya tatu lakini haikuwa siku yetu. Tunapaswa kuangalia kasoro iko wapi ili tuimarike katika siku za usoni.”

Kocha Luiz Felipe Scolari ambaye sasa anakabiliwa na shinikizo la kumtaka ajiuzulu, alisema mambo yalianza kuharibika baada ya goli la mapema. Ilikuwa mara ya nne ambapo Brazil imecheza katika mchuano wa kumtafuta mshindi wa tatu. Iliipiku Sweden mwaka 1938 na Italia 1978, na ikazidiwa nguvu na Poland katika mwaka wa 1974. Uholanzi ilicheza mchuano wa nafasi ya tatu katika mwaka wa 1998, ambapo ilishindwa na Croatia magoli mawili kwa moja, baada ya kupigwa na Brazil katika nusu fainali.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba