Uholanzi yaizuwia Ujerumani
12 Julai 2013Mabingwa watetezi Ujerumani walitoka sare ya bila kufungana na Uholanzi siku ya Alhamis katika mchezo wao wa ufunguzi katika kundi B la mashindano ya ubingwa wa mataifa ya Ulaya kwa wanawake nchini Sweden.
Katika mchezo mwingine wa kundi B Iceland ilipata bao la dakika za mwisho na kupata point moja muhimu katika mchezo uliotoka sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Norway. Hakuna timu ambayo imeweza kupata ushindi katika fainali hizi za kombe la mataifa ya Ulaya kwa wanawake hadi sasa, baada ya wenyeji Sweden kutoka sare na Denmark na Italia ikatoka sare pia na Finland katika kundi A.
Pep aishutumu Barca
Kocha mpya wa Bayern Munich Pep Guardiola amezusha kimbunga katika vyombo vya habari nchini Uhispania wiki hii baada ya kuwashutumu waajiri wake wa zamani Barcelona kwa kujaribu kutumia ugonjwa wa kocha Tito Vilanova kumshutumu.
kocha huyo mwenye umri wa miaka 42, ambaye ameshinda mataji 14 kati ya mwaka 2008 na 2012 akiwa na Barcelona na akawa na mapumziko ya mwaka mmoja mjini New York kabla ya kujiunga na vigogo wa soka la Ujerumani Bayern Munich , ameweka wazi mpasuko kati yake na rais wa Barca Sandro Rosell pamoja na kikosi chake kizima cha uongozi.
Makamu wa rais wa Barcelona hata hivyo amesema amestushwa aliposikia matamshi ya Guardiola na amekana kuwa klabu hiyo imetoa madai dhidi yake.
Usajili
Klabu ya Serie A nchini Italia ya Napoli imepata saini ya mshambuliaji kutoka Hispania Jose Callejon kutoka klabu ya Real Madrid. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26, ambaye ametokea katika academi ya soka ya Real ataitumikia klabu hiyo kwa muda wa miaka minne.
Wakenya wameingiwa na shauku kubwa baada ya mchezaji wa tiumu ya taifa ya Kenya Harambee Stars Victor Wanyama kumwaga wino kwa klabu ya Premier League ya Southampton kutoka Celtic ya Scottland kwa kitita cha pauni za Uingereza milioni 12.5. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 amekubali mkataba wa miaka minne.
Shirikisho la soka nchini Kenya lilikuwa la kwanza kumpongeza Wanyama , likisema Wanyama , ambaye alichukua wadhifa wa nahodha wa Harambee Stars kutoka kwa Dennis Oliech Juni mwaka huu, ameendelea kuwa balozi mzuri wa Kenya katika soka kutokana na jinsi anavyofanya mambo yake uwanjani.
Je Rooney atahama ManU
Wayne Rooney anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa mwezi mmoja baada ya kupata maumivu katika mguu wake wakati wa mazowezi kabla ya mchezo wa kirafiki kati ya Manchester United na Thailand All Stars.
Ronney amerejea nchini Uingereza asubuhi ya Ijumaa, lakini uvumi unasema huenda anaishinikiza klabu hiyo ili imuuze katika klabu nyingine. Uvumi huo unaongezwa na ukweli kwamba Rooney hajisikii vizuri hivi sasa na kikosi cha kocha mpya David Moyes na kocha wa Chelsea ambako anasemekana anataka kuhamia Jose Mourinho amekiri kuwa anampenda sana sana wayne Rooney.
Mourinho hata hivyo amesita kusema iwapo anamatumaini ya kumsajili nyota huyo wa Manchester United.
Kocha wa Afrika kusini Gordon Igesund anaihofia Namibia wakati timu hizo zinakaribia kuumana katika robo fainali ya kombe la Cosafa nchini Zambia leo jioni. Namibia iliishangaza Bafana Bafana mara mbili katika michezo hiyo huko nyuma ya kuwania ubingwa wa mataifa ya kusini mwa Afrika.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / ape / rtre
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman