1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhispania yaondoa vizuizi vya COVID-19

21 Juni 2020

Uhispania imeondoa vizuizi vilivyoweka nchini humo ili kukabiliana kusambaa kwa virusi vya corona na kuwaruhusu watu kusafiri tena kwa uhuru kwenye maeneo yote ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3e7Ky
Spanien Coronavirus Grenzöffnung
Picha: Getty Images/AFP/J. Lago

Marufuku hiyo imeondolewa baada ya kutekelezwa kwa muda wa wiki 14, ambapo wananchi walitakiwa kusalia nyumbani. Hata hivyo Uhispania moja ya nchi zilizoathirika vibaya na virusi vya corona, imesema masharti mengine kama vile kuvaa barakoa kwenye maduka, viwanja vya ndege na kwenye usafiri wa umma na kwenye maeneo mengine ya wazi yataendelea.

Idadi ya watu waliokufa kutokana na virusi vya corona nchini Uhispania ni zaidi ya 28,000 na zaidi ya watu 245,000 wameambukizwa virusi hivyo. Shule nchini Uhispania zitafunguliwa tena mwezi Septemba. Watalii kutoka nchi za eneo la Schengen lisilo na mipaka wanaruhusiwa kuingia tena Uhispania, huku wasafiri kutoka kwengineko ulimwenguni wataanza kuingia nchini humo kuanzia Julai Mosi.

Marekani yatakiwa kupunguza upimaji

Wakati huo huo, Rais wa Marekani, Donald Trump amewataka maafisa wa afya kupunguza kasi ya kuwapima watu virusi vya corona. Akizungumza katika wa kuzinduliwa kwa kampeni yake kuwania kuchaguliwa tena kwenye uchaguzi wa Novemba, Trump amesema maafisa wa afya waachane na mpango huo kwani unasababisha kuongezeka kwa idadi kubwa ya visa vya maambukizi.

''Unapowapima watu kwa wingi, utabaini watu wengi zaidi wameambukizwa. Hivyo nawaambia watu wangu, tafadhali punguzeni kasi ya upimaji wa COVID-19. nyie mnapima nakupima tu,'' alisema Trump. Aidha, Trump ameongeza kusema kuwa Marekani imewapima watu milioni 25 virusi vya corona.

USA Wahlkampfveranstaltung Trump in Tulsa
Rais wa Marekani, Donald TrumpPicha: Getty Images/W. McNamee

Nako nchini Iran, shirika la habari la Iran, Isna limeripoti kuwa Waziri wa Afya Saeed Namaki amesema mripuko wa virusi vya corona utaendelea hdi 2022. Namaki amesema kulingana na makadirio rasmi, wananchi wa Iran itabidi waishi na virusi vya corona kwa miaka mingine miwili.

Iran inakabiliwa na mripuko mbaya wa COVID-19 katika eneo la Mashariki ya Kati, huku kukiwa na uvumi kuhusu takwimu rasmi za waathirika pamoja na maafisa wa ngazi ya juu wa serikali ambao wanaugua na kufariki kutokana na virusi hivyo.

Maambukizi Urusi

Urusi kwa upande wake imerekodi visa vipya 7,728 vya virusi vya corona na kuifanya idadi jumla ya wagonjwa kufikia 584,680. Idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na siku ya Jumamosi ambayo ilikuwa visa 7,889, takwimu zinazoendana na siku za nyuma. Urusi pia imerekodi vifo vipya 109 na kuifanya idadi jumla ya watu waliokufa kwa COVID-19 kufikia 8,111.

China imeripoti visa vipya 25 vya virusi vya corona, 22 vikiwa ni kutoka Beijing, kutokana na juhudi za kuwapima watu milioni mbili. Idadi ya maabukizi ya wimbi jipya mjini Beijing imezusha hofu ya kuibuka tena kwa virusi hivyo nchini China, ambako katika siku zilizopita ilirekodi visa vipya kwa tarakimu moja.

Maeneo mengi yamefungwa Beijing ili kuzuia kusambaa kwa COVID-19, huku shule zikiendelea kufungwa na wakaazi wametakiwa kuepuka safari zisizo za lazima. Hadi sasa zaidi ya watu 220 wameambukizwa virusi vya corona katika wimbi jipya la maambukizi. Shirika la habari la China, Xinhua limeripoti kuwa maafisa wa Beijing wameanzisha zaidi ya vituo 2,000 vya kupima virusi vya corona kwenye mji huo ili kufanya vipimo vingi.

Coronavirus | China Peking Großmarkt von Yuegezhuang Desinfektion-Team
Maafisa wa afya wakinyunyizia dawa kwenye soko la Yuegezhuang, BeijingPicha: picture-alliance/Xinhua/Chen Zhonghao

Nchini Ujerumani, visa vipya 687 vimeripotiwa siku ya Jumapili na kuifanya idadi jumla ya maambukizi  kufikia 189,822. Takwimu hizo ni kulingana na Taasisi ya Robert Koch. Visa hivyo ni vya juu ikilinganishwa na siku iliyotangulia, ambapo walirekodiwa wagonjwa wapya 601. Taasisi hiyo pia imeripoti kwamba idadi ya vifo vilivyotokana na virusi vya corona nchini Ujerumani ni 8,882.

Wakati hayo yakijiri, Umoja wa Mataifa umetoa ripoti maalum inayoelezea wasiwasi kuhusu kile ilichokiita ''mashambulizi ya makusudi'' dhidi ya wafanyakazi wa huduma za afya na vituo vya afya nchini Afghanistan wakati wa janga la COVID-19. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Mpango wa Usaidizi nchini Afghanistan, UNAMA umesema umerekodi matukio 12 ya vitendo vya makusudi vya ghasia kati ya Machi 11 na Mei 23.

Mashambulizi yafanywa na Taliban na serikali

Ripoti hiyo imesema matukio manane kati ya hayo yalifanywa na wapiganaji wa Taliban, huku matatu yakifanywa na vikosi vya usalama vya Afghanistan. Mkuu wa UNAMA, Deborah Lyons amesema wakati ambapo msaada wa dharura wa kibinaadamu ulikuwa ukihitajika ili kuyalinda maisha ya kila raia wa Afghanistan, Taliban na vikosi vya serikali vimefanya mashambulizi ya makusudi ambayo yamedhoofisha shughuli za afya.

Shambulizi baya zaidi kutokea lilikuwa katika wodi ya wazazi kwenye hospitali ya Kabul mwezi uliopita ambalo liliwaua watu 24. Afghanistan imerekodi wagonjwa 28,833 wa virusi vya corona na vifo 581.

Ama kwa upande mwingine, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ametoa wito wa kulindwa kwa mazingira, baada ya kuondolewa kwa vizuizi vilivyoweka ulimwenguni kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Akizungumza na mamia ya watu waliokusanyika kwenye Uwanja wa Mtakatifu Peter siku ya Jumapili, Papa Francis amehimiza juhudi za kuilinda na kuitunza dunia ambayo imeanza tena upya kutokana na janga la COVID-19. Wanasayansi kote ulimwenguni wanafanya utafiti wa uchafuzi wa hewa na bahari kama matokeo ya kuwekwa kwa vizuizi vya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona pamoja na kufungwa kwa viwanda.

(AFP, AP, Reuters, DW https://bit.ly/2YTtBQi)