1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhispania yalivunja bunge la Catalonia

Caro Robi
28 Oktoba 2017

Waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy ameivunja serikali ya jimbo la Catalonia, bunge la jimbo hilo na ameitisha uchaguzi wa mapema utakaofanyika tarehe 21 mwezi Desemba.

https://p.dw.com/p/2mefn
Spanien PK Ministerpräsident Mariano Rajoy in Madrid
Picha: Reuters/S. Vera

Waziri mkuu wa uhispania amemnyang'anya mamlaka kiongozi wa Catalonia Carles Puigdemont na mkuu wa polisi. Hapo jana Ijumaa, baraza la Seneti la Uhispania liliipa idhini serikali ya waziri mkuu Mariano Rajoy mamlaka ya kulitawala jimbo la Catalonia moja kwa moja.

Serikali kuu ya Uhispania pia imemfuta kazi mkuu wa polisi wa Catalonia, imefunga idara ya wizara ya mambo ya nje jimboni humo na kuwasimamisha wajumbe wa Catalonia katika umoja wa Ulaya na katika serikali kuu ya Uhispania.

Bunge la Catalonia lilipitisha azimio linalotaka uhuru wa jimbo hilo kutoka Uhispania, katika hatua ya kujibu uamuzi wa Rajoy kutumia ibara ya 155 ya Katiba, inayoiruhusu serikali kuu kuchukuwa usimamizi wa maeneo yanayoasi.

Spanien Krise in Katalonien- Carles Puigdemont singt katalanische Hymne
Carles Puigdemont na wabunge baada ya kutangaza uhuru wa CataloniaPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Fernandez

Nchi nyingi zamuunga mkono Rajoy

Muungano unaotawala jimboni Catalonia wa Junts Pel Si - Pamoja kwa Ndiyo - na washirika wake wa mrengo mkali wa kushoto wa chama cha CUP waliwasilisha muswada wa azimio unaosema: "Tunaanzisha Jamhuri ya Catalonia kama taifa huru lenye mamlaka ya kidemokrasia na sheria ya kijamii. Rajoy amesema kuwa udhibiti kamili wa Catalonia ni muhimu katika kurejesha hali ya kawaida.

Mataifa mengi ikiwa ni pamoja na Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Marekani, Canada, Italia na Mexico yamesema hayatautambua uhuru wa Catalonia na badala yake yataendelea kuiunga mkono serikali kuu ya Uhispania ya waziri mkuu Mariano Rajoy.

Spika wa bunge la Umoja wa Ulaya Antonio Tajani amesema hakuna mtu atayetambua uhuru wa kujitawala wa Wacatalonia. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema anamuunga mkono kikamilifu Waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy, msimamo ambao pia umechukuliwa na Ujerumani.

Steffen Seibert, msemaji wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema uhuru wa kujitawala wa Uhispania hautatishiwa na tangazo lisilo halali la uhuru ambao utaligawanya taifa hilo na kutishia misingi yake.

EU yasema haitaruhusu Uhispania kugawika

Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Junker amesema hawataki kuuona umoja huo ukigawanyika zaidi akiongeza hataki kuona Umoja wa Ulaya ukiwa na karibu nchi wanachama 95 ifikapo kesho.

Spanien Barcelona - Befürwörter der Unabhängigkeit vor Katalanischem Regionalparlament
Wacatalonia wakisherehekea tangazo la UhuruPicha: Getty Images/Y. Herman

Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk amesema serikali ya Uhispania inaendela kuwa mshirika wa Umoja wa Ulaya na kuongeza kuwa lazima katiba iheshimiwe na hilo ni jambo lenye umuhimu wa kipekee kwa umoja huo. Umoja wa Ulaya umesimama imara nyuma ya serikali ya Uhispania katika mgogoro huo ulioanza baada ya Catalonia kufanya kura ya maoni kuhusu uhuru.

Mzozo huo wa kisiasa ulianza wakati Wacatalonia walipounga mkono uhuru kwenye kura tata ya maoni mnamo tarehe mosi mwezi huu wa Oktoba. Hatua zilizochukuliwa na Rajoy zinatarajiwa kukuabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Wacatalonia ambao maelfu walijitokeza jana kusherehekea uhuru wa jimbo hilo.

Sio kila mmoja Catalonia amefurahishwa na tangazo la uhuru wa kujitawala. Mamia ya watu wanaopinga jimbo hilo kujiondoa kutoka Uhispania waliandamana Ijumaa usiku katika mji wa Barcelona wakipeperusha bendera ya Uhispania.

Mwandishi: Caro Robi/dpa/ap

Mhariri: Zainab Aziz