1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhariri:Njia ndefu kuelekea demokrasia Misri

4 Julai 2013

Ni vyema kwamba Mursi hayuko tena madarakani. Hata hivyo kuondolewa kwake madarakani na jeshi ni sawa na kushindwa vibaya sana Misri

https://p.dw.com/p/192FQ
Mhariri wa DW: Rainer SollichPicha: DW/P. Henriksen

Kwanza Hosni Mubarak na sasa Mohammed Mursi:Kwa mara nyengine tena jeshi la Misri limeamua dakika ya mwisho kuelemea upande wa waandamanaji katika uwanja wa Tahrir na kumuondowa madarakani rais anaezidi kupoteza umaarufu-safari hii ni rais aliyechaguliwa kwa njia za kidemokrasia lakini amekuwa akizidi kuleta mfarakano kati ya jamii nchini humo.

Matokeo yake ni bayana na ya mashaka pia:Jeshi linaendelea kuwa taasisi yenye madaraka makubwa nchini Misri.Linazuwia ikilazimika nchi isiangamie.Wakati huo huo lakini wanajeshi hawafichui dhamiri yao;kwa hikma na werevu wanajitokeza kama waokozi mizozo inapotokea ili kulinda ushawishi wao mkubwa katika uwanja wa kisiasa na pia masihali yao ya kiuchumi.

Hiyo si demokrasia.Lakini demokrasia ina maana gani wakati huu nchini Misri?Umati wa watu walioandamana mnamo siku hizi za nyuma kwa sehemu kubwa kwa amani kudai Mursi ajiuzulu,wameonyesha moyo wa kijasiri na wanastahiki sifa.Hakuna mwenye kuthamini demokrasia na mfumo wa vyama vingi atakaependelea kuwa na rais katika nchi hiyo ya kiarabu yenye wakaazi wengi zaidi,mfano wa Mohammed Mursi ambae licha ya "msimamo yakini na suluhivu" aliokuwa nao hapo mwanzo,alibadilika mara moja na kuyaendeya kinyume maadili hayo na kuwaachia wafuasi wa Udugu wa kiislam wajipenyeze katika taasisi za serikali.

Jee kuna matumaini ya aina gani?

Kwamba dini ya kiislam na demokrasia vinaambatana sawa na jinsi inavyoambatana dini ya kikristo na demokrasia,hilo wengi wa waandamanaji wanakubaliano nalo.Kwamba wafuasi wa udugu wa kiislam wana msimamo waa kidemokrasia sawa na huo ,hilo wengi wanalishuku hata kama sio wafuasi wote wenye fikra kama hizo.Lakini miongoni mwao kuna wale ambao wako tayari kutumia nguvu.Na sio huko tu.Hata upande wa wapinzani wa Mursi walioteremka majiani,miongoni mwa waliberali na "wanamapinduzi",vijana waliovunjika moyo na wafuasi wa utawala wa zamani wa Mubarak,hisia za chuki na ghadhabu zinatokota.Desturi za demokrasia kote huko ni jambo geni.Hata hatua za awali kudai wafuasi wa udugu wa kiislam wachukuliwe hatua pamoja na madai chama hicho kipigwe marufuku ni ushahidi mwengine wa kasoro kubwa zilizoko.

Ni vizuri kwa Misri, Mursi hatawali tena.Kwa mtazamo wa muda mrefu ni ishara ya kutia moyo kwa eneo lote kwamba katika nchi muhimu ya ulimwenmgu wa kiarabu,wananchi walio wengi wanapaza sauti kupinga kutumiwa dini kuwakandamiza watu.Hilo nalo pia si hakika.Jamii ya Misri imegawika na hali mbaya ya kiuchumi inaweza kuchangia siku za mbele kupandisha hasira.

Kwa hivyo mashaka bado yapo:Kuingilia kati wanajeshi katika hali kama hii lilikuwa jambo la lazima hata hivyo ni pigo kwa utaratibu wa kidemokrasia nchini Misri.Pengine mapinduzi ya Misri ndio kwanza yanaanza.Na vyanzo vya matumizi zaidi ya nguvu vimejaa tele.

Mwandishi:Sollich,Rainer/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Josephat Charo