Uhaba wa nishati: Wajerumani wataka serikali kusaidia
2 Septemba 2022Kadri mfumuko wa bei unavyoongezeka ndivyo watu wanavyozidi kutoridhishwa na serikali. Hayo yanajiri huku serikali ikitangaza hatua za kupunguza matumizi ya nishati kote nchini.
Usafiri umekuwa ghali nchini Ujerumani tangu Septemba mosi. Katika miezi ya Juni, Julai na Agosti, kodi ya nishati ilipunguzwa. Aidha usafiri wa umma uligharimu euro tisa pekee kila mwezi. Lakini sasa bei ya mafuta imepanda ghafla, huku nauli kwenye treni na mabasi zikirudi kama zilivyokuwa awali. Na kana kwamba masaibu hayo hayaishi, kuna uwezekano nauli zitaendelea kuongezeka kufuatia kupanda kwa bei ya mafuta.
Wakati huo huo, kampuni za gesi na umeme zinazidi kuwatumia wateja wao taarifa kuhusu ongezeko la bei ya bidhaa hizo.
Swali kuu ambalo wengi wanajiuliza na ambalo limetawala mijadala ya umma hata kuwa ajenda ya kisiasa ni je, hali itakuwaje?
Serikali ya Ujerumani imetangaza mpango wa tatu wa ruzuku, lakini hadi sasa haijafahamika wazi utajumuisha nini?
Utafiti wa maoni: Watu wa mapato ya chini na katikati wasaidiwe
Kwa upande mwingine, utafiti uliofanywa na shirika la ARD Deutschlandtrend la Ujerumani lililokusanya maoni ya watu 1, 324 kwa kuwahoji mtandaoni na kwa njia ya simu kati ya Agosti 29 na Agosti 31, umeonesha raia wana matarajio thabiti.
Takriban nusu ya wote waliohojiwa walipendekeza ruzuku isiwe kwa wenye mapato ya chini pekee, bali hata kwa wale wenye mapato ya katikati ili kuwapunguzia mizigo, wakihoji ongezeko la bei ya bidhaa limewaathiri wote.
Moja kati ya watu watano angependa raia wasaidiwe bila kuzingatia kiwango cha kipato.
Kwa miezi mitatu iliyopita, watu waliweza kusafiri kwote Ujerumani kwa euro tisa pekee kwa mwezi kutumia treni za majimbo na mabasi. Zaidi ya tiketi milioni 52 zilinunuliwa.
Watu wengi wametamani mpango kama huo urudishwe huku 59% ya waliohojiwa wakisema wako radhi kulipa hata zaidi ya euro tisa.
Uhaba wa gesi, bidhaa ambayo nusu ya familia zote Ujerumani hutumia kupika; pamoja na kuongezeka kwa bei ya nishati, zimezusha changamoto kubwa kwa watunga sera serikalini.
Maswali ambayo ni pasua kichwa kwa watunga sera
Maswali wanayokabiliana nayo ni kama: Je ni vipi bei ya juu ya bidhaa hizo zinaweza kushughulikiwa bila ya raia walipao kodi kulemewa? Je ni kina nani haswa wanahitaji kusaidiwa? Na ni kiwango kipi cha msaada kitolewe ili kuepusha ghadhabu au machafuko ya kijamii? Wakati huohuo, shinikizo la kifedha kufuatia athari ya kuunga mkono sera ngumu ya kigeni dhidi ya Urusi, linaongezeka.
Kwa kila raia kumi, wanne sasa wanapinga vikwazo dhidi ya Urusi ikiwa vimekuwa na athari hasi na kuiongezea Ujerumani mzigo. Mtizamo huo unajitokeza zaidi mashariki mwa Ujerumani, ambayo zamani ilikuwa na uhusiano wa karibu na Umoja wa Soviet kabla ya kujiunga na Ujerumani ya Magharibi mwaka 1990.
Haijatokea katika historia ya Ujerumani kwa serikali kujikuta katika hali ya kutafuta suluhisho la matatizo mazito kama hayo kwa wakati mmoja kama ambavyo serikali ya sasa ya muungano inayoongozwa na Olaf Scholz ilivyojikuta.
Ni 31% pekee ya watu waliohojiwa ndio walisema wameridhishwa na kazi ambayo serikali ya shirikisho imefanya kushughulikia changamoto zilizoko. Idadi ambayo imezidi kushuka.
Sserikali yatangaza hatua za kupunguza matumizi ya nishati
Na sasa serikali imetangaza hatua kadhaa za kupunguza matumizi ya nishati kote nchini kwa miezi sita kuanzia Septemba mosi.
Ni pamoja na labda mabango ya biashara yanayotumia umeme kuzimwa ifikapo saa nne usiku. Taa za kurembesha majengo na sanamu kuzimwa usiku, kumbi za umma kutopashwa joto na viwango vya joto ofisini pia kupunguzwa hadi nyuzijoto 19. Hata hivyo zipo taasisi au vituo kama hospitali, shule, chekechea ambako viwango fulani vya joto vinahitajika, ambavyo vimeepushwa dhidi ya hatua hizo.
Kwa maana nyingine ni kwamba serikali inajaribu kuwahimiza raia na wafanyabiashara kutotumia nishati nyingi. Badala yake wahifadhi kiasi ili kuepusha hali ya kupungukiwa msimu wa baridi. Hayo yanajiri huku Urusi ikiendelea kupunguza kiwango cha gesi asilia inayoipa Ujerumani.
(DW)
Tafsiri: John Juma