1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugonjwa wa kipindupindu waua watu 250 Haiti

25 Oktoba 2010

Idadi ya maambukizo mapya na vifo inaelezwa kuanza kupungua na hivyo kutoa matumaini kuwa huenda ugonjwa huo ukadhibitiwa

https://p.dw.com/p/Pn9W
Watu wakibeba jeneza la jamaa yao aliyefariki dunia kutokana na kipindukipindu mjini Robine, Haiti Jumamosi Oktoba 23, 2010Picha: AP

Mkurugenzi Mkuu katika wizara ya afya nchini Haiti, Gabriel Thimote amesema kuwa idadi mpya ya watu waliokufa kutokana na ugonjwa wa kipindupindu imefikia 253 na wengine 3,115 wameambukizwa ugonjwa huo. Idadi hiyo inaonekana kuongeza vifo 33 zaidi katika kipindi cha saa 24. Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Haiti, Marie-Michele Rey amewaambia waandishi habari kuwa ugonjwa huo umeenea zaidi katika mkoa wa kaskazini wa Artibonite na maeneo ya kati ya milimani.

Lakini wasiwasi umezuka zaidi katika mji mkuu wa nchi hiyo Port-au-Prince ambako ugonjwa huo unaonekana kuwa rahisi kupenyeza katika mji huo uliozungukwa na mahema ambako maelfu ya watu wanaishi katika maeneo hayo baada ya nchi hiyo kukumbwa na tetemeko la ardhi mwezi Januari mwaka huu. Tayari imeripotiwa kuwa watu watano wameambukizwa ugonjwa huo kwenye mji wa Port-au-Prince hadi sasa. Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na uratibu wa misaada-OCHA, imesema kuwa wagonjwa hao walikuwa tayari wameambukizwa ugonjwa huo wa kipindupindu katika eneo lingine la Artibonite kabla ya kusafiri hadi Port-au-Prince.

Mkurugenzi wa afya katika mkoa huo, Dieula Louissaint amesisitiza kuwa kuna umuhimu wa kuwatenga wagonjwa wa kipindupindu ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo unaoua kwa haraka. Kiasi watu 3,000 wamelazwa katika hospitali na vituo vya afya karibu na mji wa Saint-Marc ulioko umbali wa saa chache kutoka Port-au-Prance.

Akizungumzia jinsi wanavyokabiliana na ugonjwa huo, msemaji wa Shirika la Afya Duniani-WHO, Gregory Hartl alisema, ''Tayari tuna wafanyakazi Haiti, tuna ofisi ya taifa kule. Hivyo ofisi yetu inashirikiana na makao makuu Washington kuhakikisha kuwa kila mmoja anahusika katika sekta ya afya kuisaidia Haiti kuweza kugundua haraka wagonjwa na kuwatibu haraka iwezekanavyo.''

Aidha, maafisa wamesema kuwa zaidi ya mahabusu 50 katika magereza wameambukizwa ugonjwa huo na watatu wamekufa. Rais wa Haiti, Rene Preval na Waziri wa Afya, Alex Larsen siku ya Jumamosi waliitembelea mikoa iliyokumbwa na ugonjwa huo wakati ambapo viongozi wameapa kuhakikisha maji safi na salama yanapatikana kwa wakaazi wa mikoa hiyo. Siku ya Ijumaa wizara ya afya ya Haiti iliiomba huduma za uratibu za Umoja wa Mataifa nchini humo kuchukua jukumu la kugawa dawa zilizotolewa na wafadhili wa kimataifa.

Haiti / Cholera / Kinder
Wanawake wakiwabeba watoto wanaopewa matibabu katika hospitali ya St. Nicholas mjini Saint Marc, HaitiPicha: AP

Madaktari wasio na mipaka walijenga hospitali ya muda katika mji wa Saint-Marc kwa ajili ya kuwatibu wagonjwa huku shirika la msaada la Oxfam likiwa limetuma madaktari watano wa dharura katika mkoa wa Artibonite kwa ajili ya kugawa dawa za kuweka kwenye maji, pakiti za dawa za kuongeza nguvu mwilini na vipande vya sabuni kwa zaidi ya watu 25,000. Naye Mkurugenzi Mkuu wa shirika la World Vision mjini Port-au-Prince, Sabrina Pourmand Nolen amesema shirika lake linagawa vifaa vya kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo na kwamba wanajiandaa na changamoto kwa ajili ya wiki zijazo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri:Josephat Charo