1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki yapata fedha zaidi licha ya kutotimiza masharti

Antonija Böhm9 Julai 2013

Kabla ya kwenda mapumziko ya majira ya joto, mawaziri wa fedha wa kanda inayotumia sarafu ya euro wameidhinisha awamu nyingine ya fedha za uokozi kwa Ugiriki. Lakini nchi hiyo itapaswa kutekeleza masharti kadhaa.

https://p.dw.com/p/194A6
Ugiriki
UgirikiPicha: Reuters

Ripoti ya mwisho ya wakaguzi wa pande tatu kuhusu Ugiriki ilitolewa muda mfupi kabla ya mkutano wa mawaziri wa fedha, na ilikuwa na taarifa mchanganyiko. Wakopeshaji hao, ambao ni benki kuu ya Ulaya ECB, Umoja wa Ulaya na shirikia la fedha duniani IMF, wametambua kuwa Ugiriki imepiga hatua japokuwa walisema bado kuna nafasi ya kuboresha hasa katika urasimu na ubinafsishaji wa mashrika ya serikali.

Waziri wa fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble.
Waziri wa fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble.Picha: picture-alliance/dpa

Kutolewa kwa awamu ya pili ya mkopo kulitegemea ripoti hiyo. Lakini licha ya kuwepo na kasoro kadhaa, mawaziri wa fedha walikubali kuipa Ugiriki fedha nyingine kiasi cha euro bilioni 6.8 kutoka mfuko wa uokozi. Ugiriki inatakiwa kufanya mageuzi zaidi ya kodi na kupunguza maelfu ya wafanyakazi wa umma kabla haijapatiwa fedha nyingine.

Ucheleweshaji hausaidii

Ni ajabu kuwa wakosoaji wawili wakubwa walikuwa wakarimu sana kwa Ugiriki mara hii mjini Brussels. Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble alizungumza kwa upole,"kwamba mambo nchini Ugiriki ni magumu si jambo geni,". Lakini alisema nchi hiyo imepiga hatua. "Nina uhakika tutaendelea na njia hii ngumu lakini yenye mafanikio kwa Ugiriki katika miezi ijayo."

Mwenzake kutoka Austria, Maria Fekter naye anayaona mambo katika mtizamo huo. "Ukuaji wa uchumi umekuwa mzuri kuliko ilivyotarajiwa," alisema. "Utalii unapanda juu, na wanatakiwa tu kuendelea na mageuzi ya kimuundo."

Alikuwa ni Fekter aliesisitiza huko nyuma kuwa masharti yote lazima yatekelezwe kwanza, pale Ugiriki iliposhindwa kutekeleza mageuzi kwa wakati, au kutotekeleza kabisaa. Misimamo yake ilikuwa ikisababisha kuzuwia kwa fedha hadi muda wa mwisho, ili tu kuongeza shinikizo kwa utawala mjini Athens. Lakini safari hii inaonekana alibadili fikira zake.

Waziri wa fedha wa Austria, Maria Fekter.
Waziri wa fedha wa Austria, Maria Fekter.Picha: picture alliance/Herbert Neubauer

"Nadhani ni jambo zuri kuwa tunafanya uamuzi hapa na leo, na si kama ilivyokuwa huko nyuma. Nadhani mbinu za ucheleweshaji zinatuongezea gharama badala ya kutusaidia," alisema kabla ya kutumaini kuwa mapumziko yajayo yatakuwa na utulivu. " Sitaki kulaazimika kurudi tena mjini Brussels, itakuwa vizuri kama tutaonana tena katika majira ya mapukutiko," alisema waziri huyo.

Mgogoro wa Ureno waisha

Mawaziri hao walionekana kuridhika kwamba mgogoro wa serikali nchini Ureno umemalizika. Mgogoro huo ulisababishwa na kujiuzulu kwa waziri wa fedha Viktor Gaspar wiki iliyopita, ambaye alisema kuwa anahisi umma hauungi tena mkono hatua zake za kukaza mkwiji. Hatua yake hiyo ilisababisha kupanda kwa kiwango cha riba kwenye dhamana za serikali ya Ureno. Hata hivyo, serikali ya muungano ya waziri mkuu Pedro Passos Coelho kwa sasa imeimarika.

Hata waziri Schäuble aliipuuza hatari hiyo. "Migogoro ya kiserikali inatokea mara kwa mara katika nchi wanachama," alisema na kuongeza kuwa hakushangazwa na kujiuzulua kwa mwenzake mjini Lisbon, lakini alisikitishwa na hatua yake hiyo. Alisema anatiwa moyo na utulivu ulionyeshwa na Ureno katika miaka ya hivi karibuni, na kuongeza kuwa nchi hiyo inapaswa kuendelea na njia hiyo. Njia ya Ureno inaweza kuwa ni yenye mafanikio katika muktadha ya fedha za uokozi, lakini iwapo raia watafuata njia hiyo mwisho ni jambo lingine.

Rais wa benki kuu ya Ulaya ECB, Mario Draghi.
Rais wa benki kuu ya Ulaya ECB, Mario Draghi.Picha: Daniel Roland/AFP/Getty Images

Draghi akosoa

Alikuwa ni rais wa benki kuu ya Ulaya Mario Draghi aliyemwaga maji katika mvinyo wa mawaziri hao. Draghi hakuzungumza wakati mmoja na mawaziri hao, bali alizungumza mbele ya kamati ya fedha na uchumi ya bunge la Ulaya. Lakini ujumbe wake uliwalenga moja kwa moja mawaziri hao wa fedha.

Tatizo kubwa zaidi barani Ulaya, alisema Mtaliana huyo, ni mdororo wa kiuchumi. "Shughuli za kiuchumi katika kanda inayotumia sarafu ya euro zimepungua kwa robo ya sita mfululizo mwaka huu wa 2013, na hali katika soko la ajira inaendelea kuwa dhoofu.

Hatari nyingine zinahusisha kupungua kusikotarajiwa kwa ulaji, na kasi ndogo au duni ya utekelezaji wa mageuzi ya kimuundo katika nchi za kanda inayotumia sarafu ya euro. Ujumbe wake ulikuwa: Hapana, hakuna haja ya kuhofu, lakini hatupaswi kujisahau wakati wa mapumziko ya majira ya joto.

Mwandishi: Christoph Hasselbach
Tafsiri: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Daniel Gakuba